Na Mwandishi wetu, Babati
MBUNGE wa Jimbo la Babati Mjini Mkoani Manyara, Pauline Philip Gekul (CCM) amekabidhi bati 30 za kupaulia jengo la Tawi la CCM Maisaka A.
Gekul amekabidhi bati hizo mara baada ya kufanya kikao cha ndani na viongozi wa CCM Tawi la Maisaka A mjini Babati.
Awali akiwa katika kikao hicho Mhe Pauline Gekul aliombwa mabati 30 kwa ajili ya kupaua ofisi ya Tawi ombi ambalo alilikubali na kulitekeleza kwa kutoa bati 30 zenye thaman ya shilingi 750,000.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi hao wa Tawi, Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa ofisi hiyo Joyce Mdee ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Babati Mjini amemshukuru Mbunge huyo kwa kuweza kuchangia mabati hayo.
Joyce amesema viongozi na wanachama wa Tawi la Maisaka A wanatoa shukrani za dhati kwa mbunge huyo kwa kutekeleza ombi lao la kupaua ofisi hiyo ambayo itakuwa inatoa huduma kwa wanachama wote.
Pia mjumbe huyo ametoa wito kwa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kufanya siasa za kistaarabu badala ya kufanya siasa za kuchafuana.