Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), akisikiliza maelezo ya msaada huo kutoka kwa Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa suti ya kijivu) na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (aliyevaa shati jeupe), wakifurahia picha ya pamoja na wawakilishi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na wakandarasi wakati wa makabidhiano ya msaada uliotolewa na mgodi huo kwa ajili ya waathirika wa maafa ya mvua mjini Musoma leo Aprili 17, 2025.
————————————
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na baadhi ya wakandarasi wanaofanya nao kazi, umetoa msaada fedha taslimu na bidhaa mbalimbali kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na maafa ya mvua katika mji wa Musoma.
Mgodi huo umekabidhi shilingi milioni 45.2, saruji mifuko 200 na magodoro 20 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi mjini Musoma leo Aprili 17, 2025.
Msaada huo kutoka Barrick umekuja wiki chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya kibinadamu ya wakazi wa mji wa Musoma walioathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na kimbunga hivi karibuni.
Akizungumza mbele ya timu ya wafanyakazi kutoka mgodi wa North Mara ikiongozwa na Meneja Mahusiano, Francis Uhadi na msaidizi wake, Nasieku Kisambu, Kanali Mtambi ameushukuru mgodi huo na wakandarasi hao kwa msaada huo.
Kiongozi huyo amesema anaona fahari mkoa huo kuwa na wawekezaji kama Barrick wanaojali maisha ya watu wenye uhitaji kama kampuni.
“Ninawashukuru sana Barrick na wadau wengine. Huu ndio Utanzania, na mimi kama Mkuu wa Mkoa najisikia fahari kwa uwepo wenu. Siwezi kupata maneno mazuri ya kuelezea shukrani zangu kwa sababu hali ya waathirika ilikuwa mbaya sana,” amesema.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Kanali Mtambi ameahidi kushirikiana na kamati husika kuhakikisha kuwa msaada huo kutoka Barrick unawafikia walengwa kwa ukamilifu.
Kwa mujibu wa Kanali Mtambi, baadhi ya waathirika wa maafa hayo wamekamilishiwa mahitaji na wengine bado wanahitaji misaada mbalimbali ya kibinadamu.
Kanali Mtambi amefafanua kuwa waliokamilishiwa mahitaji muhimu ni pamoja na wazee wasiojiweza, wakiwemo waliojengewa nyumba za makazi.
Amesema miundombinu ya umeme na barabara iliyoharibiwa na mvua hiyo imeshafanyiwa matengenezo na kurejeshwa katika hali ya kawaida.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema mvua iliyoambatana na kimbunga iliezua paa za majengo ya makazi ya watu, biashara na taasisi mbalimbali, zikiwemo shule za msingi, kituo cha polisi, msikiti na kuharibu baadhi ya miundombinu ya umeme na barabara.