Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed O.Mchengerwa akiwasilisha Makadirio ya mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Aprili 16, 2025 Bungeni Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed O.Mchengerwa akiwasilisha Makadirio ya mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Aprili 16, 2025 Bungeni Jijini Dodoma.
OR-TAMISEMI
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imewasilisha bungeni makadirio ya mapato kwa mwaka 2025/26 yenye takribani Shilingi trilioni 11. 783 kwa ajili ya wizara na taasisi zilizo chini yake.
Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 10.125 zilizotengwa mwaka 2024/25 hadi kufikia Shilingi trilioni 11.783 na kuwa na ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 1.66.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa iamesema Shilingi trilioni 3.95 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 2.5 ni fedha za ndani, ikijumuisha Shilingi bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri na Shilingi trilioni 1.45 ni fedha za nje.
Pia amesema Shilingi trilioni 7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida yanayojumuisha mishahara Shilingi trilioni 6.3 na matumizi mengineyo Shilingi trilioni 1.53 ikijumuisha Shilingi trilioni 1. 067 za mapato ya ndani ya halmashauri.
“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika. TAMISEMI haitafuti sifa ya kisiasa, tunatafuta suluhisho sahihi kwa maisha ya mtanzania wa kawaida.”
Aidha, Mchengerwa ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana, kusonga mbele kwa mshikamano.
“Kwa dhamira hii, na kwa imani kubwa katika maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii.”
“Kwa hiyo, tunasema kwa ujasiri mkubwa, TAMISEMI, ndiyo msingi wa maendeleo endelevu. Kila Shilingi ina Jukumu, Kila Kiongozi ana Wajibu na Kila Mwananchi ana Nafasi!”