Baadhi ya Wakulima wa kahawa kijiji cha Liyombo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Afisa Ushirika wa Halmashauri hiyo Nuhu Serenge kushoto kuhusu umuhimu wa kuondoa majani yasiyofaa kwenye mashamba ya kahawa ili kuepuka kuambukiza magonjwa mbalimbali yanayosababisha kupunguza ubora wa zao hilo.
Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Nuhu Serenge kushoto,akiwaelekeza baadhi ya Wakulima wa zao la kahawa wa kijiji cha Liyombo kata ya Linda namna ya kuondoa uchafu na majani yasiyohitajika kwenye zao la kahawa wakati wa ziara ya kuwatembelea wakulima wanaojihusisha na kilimo cha zao hilo jana,kulia mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Liyombo Amcos Josephat Mbele.
Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Nuhu Serenge kushoto,akikagua moja ya shamba la mkulima wa kahawa katika kijiji cha Liyombo kata ya Linda jana wakati alipowatembelea wakulima wa kahawa katika kijiji hicho.
Baadhi ya Wakulima wa kijiji cha Liyombo kata ya Linda Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakiondoa majani na wadudu wanaoharibu kahawa katika moja ya shamba la mkulima wa kijiji hicho.
Na Mwandishi Wetu-Mbinga
TANI zaidi ya 1,271 za kahawa zimezalishwa na kukusanywa kupitia Chama cha Msingi cha Liyombo Amcos Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma katika msimu wa kilimo 2024/2025 huku Wakulima wanaohudumiwa na Chama hicho wakijipatia Sh.bilioni 10,965,241,344.3.
Katibu wa Chama cha Liyombo Amcos Angelina Nchimbi alisema,uzalishaji huo ni mkubwa tangu Chama hicho kilipoanzishwa ikilinganisha na msimu wa kilimo 2023/2024 ambao wakulima walizalisha na kuuza tani 309 zenye thamani ya Sh.bilioni 1,585,941,824.
Nchimbi alisema,Chama cha msingi Liyombo Amcos kimeanzishwa mwaka 2019 na kinafanyakazi ya kukusanya kahawa kutoka kwa wanachama wake na kutafuta soko la pamoja na kuzuuza kwa mfumo wa stakabadhi mazao ghalani ambao umeleta manufaa makubwa kwa wakulima wa zao hilo.
Alisema,Chama kwa kushirikiana na wakulima kimefanikiwa kuongeza uzalishaji wa kahawa kwani takwimu zinaonesha tangu kiliposajiliwa mavumo yameongezeka kutokana na huduma wanazopata kutoka Serikalini ikiwemo mbolea za ruzuku zinazouzwa kwa bei ndogo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Liyombo Joseph Mbele,ametaja baadhi ya huduma wanazopata pamoja ni mikopo ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa mbolea,dawa za kuuwa wadudu na magonjwa ya kahawa.
“katika msimu wa kilimo 2023/2024 tuliidhinishiwa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma kukopa Sh.milioni 180 kwa ajili ya kununua pembejeo pamoja na fedha za malipo ya awali na msimu 2024/2025 tumeidhinishiwa kukopa Sh.milioni 350”alisema Mbele.
Ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma kwa kuwahidhinishia mikopo ambayo imewaletea ufanisi mkubwa kwani bila mikopo hiyo wasingeweza kufanya shughuli za kilimo kwa tija.
Aidha alisema,kabla ya kuanzishwa Amcos wakulima walikuwa na hali mbaya kiuchumi kwani walishindwa kuzalisha kwa tija kutokana pembejeo kuuzwa kwa bei kubwa na kukosa mahali sahihi kwa ajili ya kuhifadhi kahawa wanazozalishaji.
“baada ya kuanzishwa kwa Amcos sasa wakulima wanashirikiana na Uongozi wa Bodi ya Chama chetu kukusanya kahawa na kuzihifadhi gharani kabla ya kuzipeleka kwa Chama Kikuu cha Ushirika Mbinga(Mbifacu)kwa ajili ya kuuza kupitia mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani”alisema.
Mwenyekiti kitengo cha uzalishaji wa Amcos hiyo Yukundus Hyera alisema,kabla Serikali haijaanza kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo mashamba yao hayakuwa mazuri kwa kuwa walishindwa kuyahudumia vizuri.
Alisema,baada ya Serikali kuanza kutoa ruzuku kwenye pembejeo uzalishaji umeongezeka mara mbili zaidi na wakulima wameanza kufurahia matunda ya Serikali yao ya awamu ya sita kwa kupata mavuno mengi na bei nzuri ya kahawa.
Hyera,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia wakulima hasa upatikanaji rahisi wa pembejeo zinazouzwa kwa bei ndogo ikilinganishwa na hapo awali ambapo pembejeo ziliuzwa kwa bei kubwa iliyopelekea baadhi ya wakulima kushindwa kuhudumia mashamba yao.
Mkulima wa kahawa wa kijiji hicho Renigus Komba,ameishukuru Serikali kwa kusimamia zao la kahawa hasa katika kipindi cha miaka mitatu toka kuanzishwa kwa Chama cha msingi cha Ushirika Liyombo.
Alisema,kabla ya kujiunga kwenye ushirika wakulima waliuza kahawa kwa bei ya ndogo ya Sh.3,000 kwa kilo moja lakini baada ya Serikali kusimamia bei ya kahawa kwenye masoko ya nje na kuondoa baadhi ya tozo wanauza kahawa kwa Sh.8,500 hadi 9,000.