Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jacqueline Ngonyani, aliyetaka kujua kuwa Serikali ina mpango gani wa kupunguza Tozo na Kodi za uingizaji wa samaki toka nje ya nchi.
Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesema kuwa kupitia Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) katika vikao vyake, inaendelea kupokea mapendekezo yanayowasilishwa na wadau kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jacqueline Ngonyani, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupunguza Tozo na Kodi za uingizaji wa samaki toka nje ya nchi.
‘‘Tathmini ya kina hufanyika ili kubaini hali ya soko, tabia za walaji, mahitaji, gharama, athari kwa mapato ya Serikali na kuzingatia umuhimu wa kulinda walaji na wafanyabiashara wa ndani ili kuongeza mchango wa thamani katika mnyororo wa Uchumi’’, alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande aliongeza kuwa maamuzi na mapendekezo ya kupunguza tozo na kodi za uingizaji wa samaki kutoka nje ya nchi yatafanywa kulingana na matokeo ya tathmini husika.