Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), amefanya ziara ya kikazi ya siku moja tarehe 3 Aprili 2025 katika Kikosi cha Ruvu JKT ili kujionea utekelezaji wa matumizi ya nishati safi.
Akiwa kikosini hapo, Mheshimiwa Waziri alipata fursa ya kutembelea jiko la kikosi na kushuhudia jinsi nishati safi inavyotumika. Ametoa pongezi kwa Mkuu wa Kikosi kwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati.
Akizungumza na uongozi wa kikosi, Dkt. Tax amesema kuwa ziara yake imelenga kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Nishati Safi wa Taifa, ambao unasimamiwa kwa karibu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kuwa taifa linatumia nishati safi.
Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa, taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 zinapaswa kufikia matumizi ya nishati safi kwa asilimia 100 ifikapo Aprili 2025. Amesisitiza kuwa Vikosi vya JKT na baadhi ya vikosi vya JWTZ ni miongoni mwa taasisi zinazolisha idadi kubwa ya watu, hivyo utekelezaji wake ni wa muhimu.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT amepongeza uongozi wa Kikosi cha Ruvu JKT chini ya Kamanda wa Kikosi, Kanali Mnyani, pamoja na usimamizi wa Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, na watendaji wao kwa juhudi kubwa wanazofanya.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa mpango huu si tu kwamba unalinda mazingira, bali pia unaokoa fedha nyingi, ambapo kwa makadirio, kiasi cha takribani shilingi bilioni saba kitaokolewa katika vikosi vyote nchini.
Mheshimiwa Waziri alihitimisha ziara yake kwa kutembelea eneo la hifadhi ya wanyama ndani ya kikosi, ambapo aliwasihi Watanzania kutembelea maeneo hayo ili kushuhudia ubunifu na utunzaji wa mazingira.

