Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Pendo Damas,akizungumza kwenye hafla ya utiliaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji katika kata nane za Wilaya hiyo,katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Mji wa Mbinga(Mbiuwasa)Mhandisi Yonas Ndomba na Mkuu wa Wilaya hiyo Kisare Makori.
Baadhi ya Wenyeviti wa mitaa Halamshauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wakifuatilia zoezi la utiliaji saini mkataba ya ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika kata nane za Wilaya ya Mbinga.
Na Mwandishi Maalum,Mbinga
BAADHI ya wakazi wa kata ya Masumuni Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kutoa Sh.bilioni 4 ili kuboresha huduma ya majisafi na salama kwenye kata nane ikiwemo ya Masumuni.
Wamesema,hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika kata ya Masumuni siyo ya kurudhisha kwani wanapata kwa mgao hivyo kuathiri shughuli zao za maendeleo na wakati mwingine wanalazimika kwenda mbali na makazi yao kufuata maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Mkazi wa kata ya Masumuni Moses Mdaka Mapunda alisema,tangu Mji wa Mbinga ulipoanzishwa hawajawahi kupata fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji badala yake walikuwa na miradi midogo ambayo kwa sasa imeshindwa kukata kiu ya maji kwa Wananchi wa Mji wa Mbinga.
Mapunda,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali Wananchi wa Mbinga, kwani mradi utakapokamilika utamaliza tatizo la huduma ya maji kwa wakazi wa kata hiyo na kata nyingine chenye changamoto hiyo katika mji wa Mbinga.
Aidha Moses Mapunda,amemtaka Mkandarasi aliyepewa kazi ya kutekeleza mradi huo kampuni ya Ngongo Engineering Ltd kuhakikisha anafanya kazi kwa wakati na ubora ili waweze kupata maji kwani fedha za mradi huo zipo.
“kama nilivyosema awali haijawahi kutokea mji wetu wa Mbinga kupata mradi mkubwa wa maji kama huu,naiomba Serikali kupitia Mbiuwasa imsimamie kwa karibu Mkandarasi ili akamilishe kazi haraka na sisi wananchi tupate maji kwenye maeneo yetu”alisema Mapunda.
Mkazi mwingine wa mtaa huo John Yapesa,ameishukuru Serikali kuleta mradi huo ambao unakwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Mji wa Mbinga ambao unakuwa kwa kasi kubwa.
Yapesa ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi tawi la Masumuni,amemtaka Mkandarasi kuanza kazi haraka na kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi aliyopewa kwani katika kata hiyo kuna changamoto kubwa ya huduma ya maji.
Alisema,kwa sasa wanawake na watoto wanatembea umbali mrefu kwenda mtoni kutafuta maji na wakati mwingine wanatumia muda mwingi kukaa kwenye vituo vya kuchotea maji hali inayorudisha nyuma maendeleo yao.
Mkazi wa mtaa wa Lusaka Fides Ngonyani,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuboresha huduma ya maji katika mji wa Mbinga.
Amemuomba Mkandarasi,kuhakikisha anapanua mtandao wa mabomba kwenye mitaa mbalimbali ili kuwarahisishia wananchi kupata maji kwenye makazi yao badala ya kuendelea kuteseka kwa kupata maji ya mgao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga Pendo Damas,amewaomba Wananchi kutunza mradi na kulinda vyanzo vya maji ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbinga Ali Simba alisema,mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kuipongeza Serikali kwa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani.
Simba,amewataka wananchi wa Mbinga na Watanzania kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali iliyopo madarakani kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji inayotekelezwa kwa lengo la kuharakisha kuboresha maisha ya Wananchi na kukuza uchumi.
Serikali kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mji wa Mbinga(Mbiuwasa)imeingia mkataba na Mkandarasi kampuni ya Ngogo Engineering Ltd kwa ajili kujenga mradi wa kuboresha huduma ya maji katika mji huo utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 12.