Na Mwandishi wetu, Mirerani
MAMIA ya wakazi wa Mikoa ya Manyara, Arusha, Singida na Kilimanjaro, wameshiriki kwenye harusi ya Rogers Elisha na Angel, mtoto wa Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi.
Ndoa takatifu imefungwa na Askofu Sommy Severua wa Desciple Nations Pentecost Church (DNPC) Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro na sherehe za harusi zimefanyika kwenye ukumbi wa Dream Park mji mdogo wa Boma ng’ombe, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza wakati akitoa nasaha zake, Mwenyekiti wa MAREMA, Elisha Nelson Mnyawi amemweleza mtoto wake Rogers amtangulize Mungu kwenye kila jambo kwani kwa Mungu kuna kila kitu.
“Siku ya leo ni siku njema kwani tuliisubiri siku hii kwa muda mrefu, katika maisha yako ukimtanguliza Mungu utakula mema ya nchi, kwani kwa Mungu kuna kila jambo ukiwemo utajiri, hivyo mwanangu Mungu awe chaguo lako la kwanza,’’ amesema.
Katika sherehe ya harusi hiyo Mwenyekiti huyo wa MAREMA, Elisha Nelson Mnyawi, amemkabidhi zawadi ya shilingi milioni 10, mtoto wake kama pongezi kwa kuanza upya maisha yake ya ndoa.
“Fedha hizi zijaziweka kwenye akaunti yako benki kwa sababu nimepanda mbegu ya kukuamini na ninafahamu kuwa utaweza kuzilinda na kuzihifadhi usiku huu na kisha kuzipeleka benki wewe mwenyewe siku nyingine,” amesema.
Kwa upande wake Schola Elisha ambaye ni mama mzazi wa Rogers, amemwambia mtoto wake amtunze vyema mke wake Angel, kwani ni mama wa wajukuu zake.
“Umtunze awe na upendo na furaha na pia usisahau usia wa baba yako kuwa tafuta amani ya Mungu, nakumbuka mwanangu nilipokuzaa tulimshirikisha mchungaji Sommy Severua ili tupate jina la kukupa na akaafiki tukuite Rogers,” amesema.
Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Magreth Nelson Mnyawi, ambao ni shangazi zake Rogers, waliongozana na marafiki zao wanawake na kukabidhi zawadi ya shilingi milioni 13.2.
“Shangazi yangu Rogers sisi tumelelewa vyema na baba yetu mzee Nelson Mnyawi akitupa usia wa kuishi vizuri na watu, umeona mwenyewe hapa tumeishi kwa upendo na watu na wamesaidia kutuchangia fedha hizi za zawadi yako,” amesema Salome.
Katibu wa MAREMA, Tareq James Kibwe ambaye alimwakilisha Rais wa shirikisho la vyama vya wachimbaji nchini (FEMATA) John Wambura Bina, amewasilisha zawadi ya shilingi milioni moja, kwa ajili ya fungate ya maharusi hao.
“Rais wetu Bina alikuwa ana ratiba ya kuja kwenye harusi hii ila amepata dharura ya kikao ameenda Zanzibar ndipo akanituma nilete zawadi hiyo na salamu za maisha mema ya ndoa,” amesema Kibwe.
Hata hivyo, Kibwe alifurahisha mamia ya watu waliokuwepo kwenye sherehe hizo kwa kuzungumza lugha ya kichina na baadhi ya raia wa China waliohudhuria harusi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya usuluhishi na usalama kitalu D Barnabas Mallya amewapongeza wana ndoa hao na kuwatakia kila la heri katika maisha yao mapya.




