Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Paul Makonda akzungumza jijini Arusha leo
Happy Lazaro,Arusha .
Timu ya watoa huduma wa msaada wa Kisheria kupitia kampeni ya “Samia Legal Aid Campaign ” imeagizwa kuorodhesha majina ya watumishi wa serikali katika sekta mbalimbali watakaobainika kutajwa na wananchi kuwa wanachochea migogoro inayopelekea wananchi kuichukia Serikali.
Maagizo hayo yametolewa leo jijini Arusha na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda wakati akizungumza na wataalam wa sheria wakiwemo mawakili, maofisa maendeleo ya jamii pamoja na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali waliokutana kwaaajili ya kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto za wananchi katika halmashauri saba za Mkoa wa Arusha pamoja na kuainisha changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kila idara husika.
Amesema kunabaadhi ya maofisa maendeleo ya jamii wanalalamikiwa kwa kupindisha sheria ikiwemo watumishi wengine hivyo katika kampeni hiyo endapo kuna watumishi wanalalamikiwa kukwamisha utatuzi wa migogoro kwa wananchi wakuu wa timu husika kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waandike majina yao kisha mwisho wa kampeni hiyo watoe taarifa kwake ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Kuna baadhi ya watumishi wanatajwa na wananchi kutokana na tabia ya kukwamisha mambo tunaomba majina yao, lakini pia naomba timu hizi zianishe changamoto zote zilizoibuka ili kupelekwa mahali husika kama polisi, uhamiaji, idara ya kazi na kwingineko ili hatua stahiki zichukuliwe “
Hata hivyo, amewasihi watoa huduma hiyo kuhakikisha wanawasilikiliza wananchi wanaofika kupata msaada huo ikiwemo watoa huduma hao kujiuliza nafsini kwao je maamuzi watakayotoa ni sahihi na hakuna upendeleo ili wahusika wapate haki yao kwamujibu wa changamoto zao.
Kwa upande wake Ester Msambazi ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, amesema kampeni hiyo ilianza kutekelezwa mwaka 2023 huku Mkoa wa Arusha ukiwa ni wa 23 tangu kampeni hiyo kuanza na wamejipanga vema kuanza kutoa msaada huo.
Uzinduzi wa kampeni hiyo utafanyika Machi 28, 2025 kwenye viwanja vya Ngarenaro ambapo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk, Damas Ndumbaro na Makonda watahudhuria huku huduma na elimu za kisheria zikitolewa, utoaji wa huduma za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi pamoja na idara na ofisi mbalimbali za serikali ambazo zitatoa huduma za bure kwa wananchi na baada ya hapo timu husika zinaenda uwandani kuanza kazi rasmi Machi 29,mwaka huu.

