Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 26, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kuwasilisha mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 26, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Sehemu ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga (hayupo pichani) wakati akiwasilisha kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 26, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita,Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema hali ya uzalishaji umeme kwenye gridi ya Taifa imeongezeka mara mbili zaidi baada ya kutekeleza miradi ya ufuaji umeme maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Machi 26, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Amesema kuwa hadi kufikia mwezi Februari 2025 uwezo wa mitambo ya kufua umeme kwenye Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya Megawati 3,796.71 wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme kwenye Gridi ya umeme ya Taifa kwa yakiwa ni Megawati 1,908.
“Mwaka 2021 uwezo wetu wa kuzalisha ulikuwa megawati 1,573.6 na sasa hivi uzalishaji umeongezeka zaidi ya mara mbili ya uwezo wa kuzalisha umeme kwa kipindi kifupi cha miaka minne,” amesema Mhandisi Nyamo – Hanga
Aidha amesema kuwa wataendelea kutekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme nchini katika kuwapatia watanzania umeme wa uhakika miradi inayoendelea ya uzalishaji ni pamoja na Malagarasi MW 49.5, Kakono MW 87.8, Kishapu Solar awamu ya pili MW 100, Ruhudji Megawati MW 358 na Rumakali MW 222.
Pia amesema kuwa wataongeza zaidi ya Uzalishaji umeme wa Gesi asilia na Makaa ya mawe.
Hata hivyo amesema kuwa wataendelea na utekelezaji wa umeme kwa nishati ya jotoardhi ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania imepata mashine ya kuchoronga miamba (rig) mtambo ambao unaendelea kwa sasa kufanya kazi ya kuchoronga eneo la Ngozi Mbeya kwa lengo na kuhakiki hifadhi ya nishati ya jotoardhi, huku tafiti za awali zikionesha kunaweza kuwa na nishati ya jotoardhi yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 70 katika eneo la Ngozi Mbeya.
“Kuendelea kuimairisha miradi ya Usafirishaji na usambazaji umeme kuendana na ongezeko la mahitaji ya umeme nchini na Kuunga Mfumo wa Gridi ya Umeme ya Tanzania na nchi za Uganda, Congo, DRC, Malawi na Msumbiji” amesema Mhandisi Nyamo – Hanga
Mhandisi Nyamo – Hanga,amesema kuwa kukamilisha njia za usafirishaji umeme za Sumbawanga-katavi-Kigoma, Mkuranga-Mtwara-Kupitia Kibiti na Somangafungu na Lindi.Kukamilisha Miradi ya kusafirisha umeme ya Chalinze segera 400KV, Segera same Arusha 400kv, Segera Tanga 220 KV Chalinze Bagamoyo 220KV, Chalinze, Kinyerezi Mkuranga 400KV na ukamilishaji wa miradi ya Gridi Imara.
Vilevile kujenga Miradi ya usambazaji kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye Maeneo ya Madini, Kilimo na Viwanda.
Aidha amesema kuwa watatekeleza Mpango wa Kitaifa wa Nishati Tanzania.Serikali iliandaa na kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Nishati (African Heads of States Energy Summit) uliofanyika tarehe 27-28 Januari, 2025 Jijini Dar es salaam.
“Mkutano huo uliwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika, Wakuu wa Taasisi za Fedha za Kimataifa pamoja na Wadau wengine wa Maendeleo kwa lengo la kuweka mikakati ya namna bora ya kuwafikishia umeme watu milioni 300 katika Bara la Afrika ifikapo mwaka 2030” amesema
Pamoja na mambo mengine Mkutano huo uliwezesha kuzinduliwa kwa Mpango wa Kitaifa wa Nishati wa Tanzania (National Energy Compact 2025-2030) ambao unalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kutoka cha sasa cha asilimia 78.4 hadi kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo amesema kuwa mafanikio ya TANESCO katika kipindi cha miaka minne chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan yameleta mabadiliko makubwa katika Sekta ndogo ya Umeme Nchini.
” Wananchi wananufaika na upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa sasa Shirika linaendelea na Utekelezaji wa Miradi na maboresho mbalimbali ya miundombinu ya umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini kama nilivyoeleza ili kuhakikisha watanzania wanapata Umeme wa Uhakika ambayo ni azma kubwa ya Serikali ya awamu ya sita”amesisitiza