Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wameridhishwa na miradi yote iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora kupitia Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo Kame Nchini (LDFS).
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga tarehe 13 Machi, 2025 wilayani Nzega mkoani wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua Mradi wa LDFS unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mhe. Kiswaga ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga amesema kuwa miradi hiyo imetekelezwa kwa ufanisi na kwamba imezingatia thamani ya fedha, ubora na viwango kama inavyoelekezwa.
Aidha, amewasihi wananchi wailinde miradi inayotekelezwa na Serikali ili iendelee kuwaletea tija kwani imetumia gharama katika kuitelekeza.
Pia, amepongeza juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika miradi hiyo ili iwanufiashe wananchi.
Kwa upande Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wananchi wapande miti ili kutunza mazingira.
Amesema pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo pia wananchi wanapaswa kutunza mazingira ili kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mazingira yameharibika hivyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu miradi ya kupambana na ukame.
Amesema Wajumbe wa Kamati wanakagua maeneo ambayo miradi inatekekezwa na kwamba wananchi wanawezeshwa kufanya shughuli za kuwaingiza kipato bila kuharibu mazingira.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Sigili ambao wamenufaika na mradi wa maji akiwemo Bi. Monica Mipawa wameshukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo na kusema walikuwa wanapata changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta maji.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Kisima cha maji na mifumo ya nishati ya jua ya kusukuma maji, Ujenzi wa tenki la maji, kituo cha kuchota maji katika Kijiji cha Bulambuka Kata ya Sigili.
Miradi mingine ni kiwanda na mashine za kuchakata mazao ya nyuki, Ukaguzi wa lambo na birika la kunyweshea mifugo.