Na Farida Mangube, Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeahidi kuimarisha ushirikiano wake wa kisayansi, kielimu na kiteknolojia na Chuo Kikuu cha St. Petersburg cha Urusi katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira. Ahadi hiyo imetolewa baada ya ujio wa wataalamu 10 kutoka chuo hicho cha Urusi waliotembelea SUA kwa lengo la kutathmini na kuimarisha maeneo ya ushirikiano.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii ya SUA, Prof. Agnes Sirima, amesema kuwa ushirikiano huo utasaidia katika kubadilishana wataalamu, wanafunzi na walimu, pamoja na kushirikiana katika teknolojia za kisasa za misitu na uongezaji wa thamani ya mazao ya misitu.
“Tuna kiwanda cha samani hapa SUA, na tunatarajia kuwa ushirikiano huu utaimarisha ufundishaji wa taaluma yetu ya uchakataji wa mazao ya misitu na kuongeza thamani ya mbao,” amesema Prof. Sirima.
Ameongeza kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu kwa wataalamu na wanafunzi wa SUA kujifunza teknolojia za kisasa za upimaji wa misitu kutoka kwa wenzao wa Urusi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya satelaiti, drones, na akili bandia (AI) katika utafiti wa misitu.
Wataalamu wa Urusi pia wameeleza kuwa wanajikita katika utafiti wa uzalishaji wa miti bora, entomolojia, na usimamizi endelevu wa misitu kwa kutumia teknolojia bunifu.
Ushirikiano huu unahusisha SUA, Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), huku ukitarajiwa kuleta maendeleo chanya katika uhifadhi wa mazingira na sekta ya misitu nchini Tanzania na duniani kote.