Mbunge Viti maalum wafanyakazi Tanzania Bara, Dokta Alice Kaijage akizungumza kwenye kongamano la wafanyakazi wanawake mkoani Arusha.
Wafanyakazi wanawake wakiwa kwenye kongamano hilo lililoandaliwa na shirikisho la wafanyakazi nchini Tucta.
…………..
Happy Lazaro, Arusha .
WANAWAKE wametakiwa kuwa mstari wa mbele kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuondoa nidhamu ya uoga kwani hivi sasa kuna sheria kali inayowabana wanaume wanaodhalilisha wanawake wanaogombea katika nafasi mbalimbali.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mbunge viti maalum wafanyakazi Tanzania Bara, Dokta Alice Kaijage wakati akizungumza kwenye kongamano la wafanyakazi wanawake lililoandaliwa na shirikisho la wafanyakazi nchini Tucta.
Amesema kuwa ,wanaume ambao wamekuwa wakidhalilisha wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi watakabiliwa na sheria kali katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu 2025.
Dokta Alice amesema Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania limepitisha sheria hiyo ili kuvutia wanawake wengi kujitokeza kuwania nafasi za uongozi na kutekeleza moja ya maazimio ya Beijing.
“Matusi na udhalilishaji ni miongoni mwa vikwazo ambavyo vilikuwa vikikatisha tamaa wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi hivyo Serikali imelitambua hilo na kutengeneza sheria ya kuwakomboa,hivyo sasa hivi hawapaswi kuogopa tena badala yale wawe mstari wa mbele kuchangamkia fursa hiyo.”amesema .
Dkt. Alice amesema pia Serikali ya Rais Samia imeendelea kujali wanawake ambapo kupitia bunge la Jamhurj ya Muungano wametengeneza sheria kuwathamini wanawake wanaojifungua watoto njiti ambapo hivi sasa watakuwa wakipewa siku za kutunza watoto wao hadi umri wa kuzaliwa utakapotimia pamoja na likizo ya uzazi
Mkuu wa idara ya jinsia na wenye ulemavu kutoka shirikisho la wafanyakazi Tucta Nasra Khalid amesema lengo la kongamano hilo ni kujifunza na kujadili masuala ya wanawake kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo inafanyika kesho Jijini Arusha.
Amesema katika kongamano hilo pia wataweka mikakati ya kuweza kukabiliana na vikwazo vya kimfumo kazini ikiwemo idadi ndogo ya wanawake kwenye nafasi za uongozi.
” Mfano ukiangalia bodi ya wakurugenzi wanawake ni wachache ili kukabiliana na mambo kama haya tunatakiwa kujadiliana na kuweka mikakati, lakini pia tujenge mshikamano ndani ya Tucta,”Amesema.
Mkurugenzi wa shirika la kazi Duniani (ILO), Kanda ya Afrika Mashariki, Carolyne Mugalla amesema wanawake wamekuwa wakipitia changamoto nyingi makazini hivyo wanatakiwa kuungana na kuzitokomeza.
Amesema safari yake ya maisha hadi kufikia nafasi ya kuwa mkurugenzi wa shirika la kazi duniani Kanda ya Afrika Mashariki ilijaa vikwazo vingi lakini aliweza kupambana navyo.
” Ndugu zangu huu ni wakati wa kuunganisha nguvu moja kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo sehemu za kazi, safari yangu imetoka mbali sana hadi hapa nilipofikia, nimeruka vikwazo vingi sana,” amesema.
Kongamano hilo la siku moja lililoandaliwa na shirikisho la wafanyakazi wanawake Tanzania (Tucta), linashirikisha viongozi wanawake kutoka vyama 13 wanachama wa shirikisho hilo nchini.