Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa amefurahishwa na mwitikio wa taasisi za Serikali kwa kutenga na kutoa asilimia 30 ya bajeti za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum katika jamii.
Rais Samia ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, 8 Machi 2025, jijini Arusha.
Alisema jambo hilo limewezekana kupitia sheria mpya ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 iliyoweka sharti kwa taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya zabuni zote kwa ajili ya makundi maalum ikiwa ni pamoja na wanawake.
“Nimefurahishwa sana juzi nikiwa napokea taarifa ya Sekta ya Ujenzi na Miundombinu wakaniambia kwamba kuna kazi kadhaa za barabara zimetolewa, na asilimia 30 ya kazi hizo wamepewa wakandarasi wanawake,” alisema Rais Samia na kuelekeza kuwa hatua kama hii ifanyike kwenye maeneo mengine pia.
Inafahamika kwa wadau pia kwamba Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 inaelekeza kuwa fursa za zabuni, ikiwa ni pamoja na asilimia 30 ya bajeti ya ununuziumma katika taasisi za Serikali, itengwe kwa ajili ya makundi maalum na zitolewe kupitia Mfumo wa NeST.
Watanzania wanaweza kuunda vikundi vya watu 5 mpaka 20, vikasajiliwa kwenye halmashauri zao na baadaye kwenye NeST ili kuomba zabuni zilizotengwa kwa ajili yao.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba alisema kuwa Mfumo wa NeST, ulioanza kutumika Julai 1, 2023 ni matunda ya jitihada mahsusi za Rais Samia aliyefanikisha kupatikana kwa Sheria ya Ununuzi ya Mwaka 2023 na kutanabahisha kwamba hadi kufikia Februari 2025 makundi maalum yalipata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 11.
Pia, alieleza kuwa makundi 66 ya wanawake yalipata zabuni 146 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 5.6, na kwamba kiasi kilichobaki kimeenda kwa makundi mengine.