Afisa habari Mkuu kutoka Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) Theresa Chilambo akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao kuhusu huduma mbalimbali wanazotoa .

Afisa Usajili kutoka BRELA,Julieth Kiwelu akitoa maelezo kwa mteja aliyefika kwenye banda hilo mkoani Arusha .

Afisa Usajili kutoka BRELA Neema Shirima,akimkabidhi cheti cha usajili wa kampuni kwa mfanyabiashara wa hoteli aliyepata huduma papo kwa hapo katika maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake jijini Dar es Salaam.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.WANANCHI wametakiwa kutembelea banda la Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) katika maonesho ya kuelekea siku ya wanawake duniani ili waweze kunufaika na huduma za usajili na kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazowakabili kwani huduma imesogezwa karibu kwa ajili yao.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Afisa habari mkuu kutoka Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) Theresa Chilambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao kuhusu huduma mbalimbali wanazotoa .
Amesema kuwa kuelekea kilele cha siku ya wanawake BRELA wameshiriki ili waweze kutoa huduma hivyo ni jukumu la wananchi wenyewe kuhakikisha watumie fursa hiyo kuweza kupata elimu mbalimbali kuhusu BRELA huku lengo likiwa ni kusaidia katika urasimishwaji biashara na kutatua changamoto ,pamoja na kusajili kampuni .
Chilambo amesema kuwa, wananchi wataweza kupata elimu namna ya hatua za usajili wa alama za biashara na huduma na hatua za usajili wa hataza kwa njia ya mtandao.
“Mbali na kupata elimu.hiyo kutakuwepo na elimu juu ya hatua ya jinsi ya kuomba taarifa rasmi za kampuni na majina ya biashara kwa njia ya mtandao ,mfumo wa kielekroniki wa utoaji wa leseni za biashara na kujua hatua za kupata taarifa katika mfumo wa utoaji taarifa za taratibu za biashara za kimataifa.”amesema Chilambo.
Aidha amefafanua zaidi kuwa,mfumo wa utoaji taarifa za taratibu za biashara za kimataifa unatoa taarifa za taratibu za kupata leseni,vitality na taratibu za kiforodha kwa bidhaa zinazozafirishwa nje ya nchi ,zinazoingizwa nchini na zinazopitishwa kwenda nchi nyingine.
Amesema kuwa, mfumo wa utoaji taarifa za taratibu za biashara za kimataifa unatoa taarifa hatua kwa hatua katika mchakato wa kuomba vibali au leseni ambapo kila hatua inaonyesha wapi uende,unamuona nani,nyaraka zipi unazopaswa kwenda nazo ,fomu unazogakiwa kujaza,gharama utakazolipa,Sheria inayokuongoza katika hatua husika na mahali pa kulalamika endapo hujaridhika na huduma au kupata tatizo.
Ameongeza kuwa, taratibu zimewekwa kwa mtazamo wa upande wa mteja na sio kwa mtazamo wa upande wa Taasisi na kila mteja anapoonana na mtoa huduma inahesabika kuwa ni hatua .
Aidha amesema kuwa mbali na hiyo BRELA imekuja na kitu kipya kwa makampuni ambayo yalisajiliwa nje ya mfumo ambapo Waziri wa viwanda na biashara ametoa msamaha kwa yale makampuni ambayo yalisajiliwa nje ya mfumo kwani zamani usajili wa makampuni ulikuwa unafanywa kwa njia ya makaratasi ila kwa sasa makampuni yote yanasajiliwa kwa njia ya mfumo.
“hivyo kampuni zote ambazo zilikuwa zimesajiliwa nje ya mfumo waziri ametoa msamaha wa mwaka mmoja kampuni zijisajili kwenye mfumo na kwa gharama zote ambazo ulitakiwa ulipe utakatwa asilimia 50 ya gharama ambazo ulitakiwa kulipa lengo ni kutaka kuona kila mfanyabiashara anakuwa kwenye mfumo rasmi kwani kwa sasa BRELA inafanya kazi zake kielekroniki zaidi.”amesema Chilambo .
Aidha taasisi na wadau mbali mbali wameshiriki katika maonesho ya kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa itafanyika machi 8 katika uwanja wa Stadium mkoani Arusha .