Katika kuelekea kilele cha siku ya Wanawake Duniani, mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Arusha (TPF NET) wametumia fursa hiyo kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanafunzi na wanawake jamii ya kifugaji katika Wilaya ya Longido.
Mwenyekiti wa Mtandao huo Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Debora Lukololo wakati akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Samia Longido na Wanawake jamii ya kifugaji amesema mtandao huo umeona ni vyema kuyafikia makundi mbalimbali katika jamii hususani Wasichana na Wanawake ili kuwajengea uwezo na kuwa na uelewa wa pamoja katika utambuzi na kukabiliana na vitendo vya ukatili vinavyotendeka katika Jamii.
ACP Lukololo pia ametumia fursa hiyo kuwahamisisha Wanawake hao kujitokeza kwa wingi katika kilele cha siku ya Wanawake duniani itakayofanyika kitaifa Jijini Arusha Machi 08 mwaka huu ambapo mgeni Rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi SP Happiness Temu pamoja na kuwapa elimu juu ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, amewatahadharisha wanafunzi kuacha tabia ya kuiga tabia mbovu au vitendo viovu kutoka kwa wenzao au katika mitandao ya kijamii ambavyo havina tija kwao, badala yake wajikite katika masomo yao.
Aidha wametoa taulo za kike kwa Wanafunzi hao katika Shule hiyo ya Sekondari Samia Longido kwa ajili ya kuonesha upendo kwao kama wanawake.
Katika hatua nyingine Wanawake hao wa Polisi walipata fursa ya kutembelea kituo cha Forodha cha mpaka wa Namanga kwa upande Tanzania na Kenya kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa kazi na kujifunza namna ambavyo vituo hivyo vinafanya kazi