Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina katika picha ya pamoja na wanafunzi wa kwanza wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba iliyopo Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wakati alipotembeela na kukagua maendeleo ya ujenzi wa wa Shule hiyo tarehe 03 Machi 2025
……
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka wananchi wa Kijiji cha Kasumo na Wilaya ya Buhigwe kwa ujumla kutambua na kuthamini mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya huduma za kijamii Wilayani humo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba iliyopo katika Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma. Amesema kwa kipindi kirefu wananchi wa Kijiji cha Kasumo na maeneo jirani walisafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii lakini kwa sasa huduma hizo zimesogezwa karibu zaidi na wananchi.
Makamu wa Rais amesema ujenzi wa barabara za lami, madaraja, zahanati, shule na huduma za maji ni jitihada za serikali katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo wananchi wanapaswa kushukuru kwa kumpigia kura za ndio katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wanafunzi walioanza kusoma katika shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba kutumia vema nafasi waliyopata kusoma kwa bidii ili shule hiyo iweze kutoa wataalamu wazuri kama ilivyo kwa shule zingine kubwa nchini. Makamu wa Rais ameahidi kutoa zawadi kwa wanafunzi watano wa kwanza katika mitihani ya mwisho ya kila mwaka pamoja na walimu watakao faulisha vema masomo yao kama motisha ya wanafunzi hao kusoma kwa bidii.
Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Buhigwe kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa shule hiyo ya wasichana ambayo itakua ya kidato cha kwanza hadi cha sita kwa masomo ya sayansi. Pia, Makamu wa Rais amewapongeza wadau mbalimbali wa maendeleo Wilayani Buhigwe ambao wamekuwa wakijitolea kuiunga mkono serikali katika huduma za elimu.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kijiji cha Kasumo kutumia vema fursa ya shule hiyo iliyopatikana kwa kutunza miundombinu ya shule na kuwawezesha wanafunzi hao kupata elimu kwa amani. Amewaagiza wazazi na walezi wa Kijiji hicho kutoa kipaumbele kwa watoto kupata elimu ili Kijiji hicho kiweze kupata viongozi na wataalamu watakaotoa mchango kwa Taifa. Pia Amewataka wananchi kuwa sehemu ya maendeleo kwa kujitoa kushirikiana na serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya huduma za kijamii.
Vilevile, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wananchi hao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Amewasihi kuchagua viongozi watakaosaidia kuharakisha maendeleo pamoja na kuwaasa wale wenye sifa za uongozi kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba iliyopo Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wakati alipotembelea shule hiyo. Tarehe 03 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wanafunzi wa kwanza wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba iliyopo Buhigwe Mkoani Kigoma wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa wa Shule hiyo tarehe 03 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina katika picha ya pamoja na wanafunzi wa kwanza wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kahimba iliyopo Kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wakati alipotembeela na kukagua maendeleo ya ujenzi wa wa Shule hiyo tarehe 03 Machi 2025