NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
MANISPAA ya Ilemela imetoa sh. 1.135 za mkopo usio na riba kwa vikundi 60 vya wanawake,vijana,na watu wenye ulemavu,hatua itakayotoa fursa kubwa ya kiuchumi na kijamii kwa makundi hayo.
Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela,Mariamu Msengi,amekabidhi mikopo hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya,Hassan Masalla,leo akisisitiza matumizi sahihi ya fedha hizo ili zifanikishe malengo yaliyokusudiwa ya kuboresha hali za kiuchumi na maisha ya wanufaika.
Amesema mikopo hiyo ni jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,katika kuhamasisha maendeleo ya jamii kwa kusaidia wanawake,vijana na watu wenye ulemavu,ambao mara nyingi hukosa fursa za kifedha.
Msengi ameeleza kuwa mikopo hiyo ilisitishwa kwa muda ili kufanyiwa marekebisho,lakini sasa imerudi tena ikilenga kutoa fursa kwa makundi hayo katika jamii ambayo mara nyingi hutengwa na kuwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili wengine waweze kufaidika nayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu, amesema kuwa vikundi vya wanawake 39 vimepata sh.milioni 618, vya vijana 17 sh.milioni 492, na sh.milioni 24 kwa vikundi 4 vya watu wenye ulemavu, mkopo unaotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Amefafanua kuwa, licha ya kuwa na maombi mengi kutoka kwa vikundi 216 vikiomba fedha nyingi sh. bilioni 9 kuliko zilizokuwepo, hivyo vikundi 148 vilivyokidhi vigezo vilichaguliwa na baada ya uhakiki na ufuatiliaji, 60 vilikubaliwa kupata mikopo hiyo ingawa uhitaji ulikuwa mkubwa kuliko uwezo wa halmashauri .
“Mkopo huu wa sh. bilioni 1.135 ni hatua ya kuboresha maisha ya wanajamii walio katika hali ya chini, ni uthibitisho wa jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha usawa wa kijamii na maendeleo kwa makundi hayo katika jamii,”amesema Wayayu.
Aidha,amesema serikali inaendelea kutia mkazo uaminifu, uadilifu na matumizi bora ya fedha za umma ili kuhakikisha mikopo hiyo inawanufaisha na kuleta mabadiliko ya kimsingi katika maisha ya wanufaika.
Hata hivyo, Wayayu amesisitiza kwa sababu serikali imewekeza katika kuhakikisha mikopo hiyo inawanufaisha na inachangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.wanufaika wawe na uaminifu na uadilifu katika kurejesha mikopo hiyo, kwani ni fedha za umma hizo zina manufaa kwa jamii nzima pia, wanufaika kutokukwepa kuzirejesha fedha hizo.
Meya wa Halmashauri hiyo, Renatus Mulunga,amekumbusha mikopo hiyo kuwa haijatolewa kwa kipindi cha miaka minne, kwa sasa wanufaika wanapaswa kuonyesha uaminifu na kutumia fedha kwa manufaa yao na jamii na si vinginenvyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii,Manispaa ya Ilemela, Jonathan Mkumba,amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza ahadi ya kuwaletea wananchi maendeleo,mikopo hiyo ni kielelezo cha juhudi za serikali za kuboresha maisha ya wananchi, hasa makundi yaliyosahaulika ya wanawake,vijana na walemavu.
Amewaasa wanufaika hao kuhusu nidhamu ya matumizi ya fedha na kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili wengine pia wafaidike.
Wanufaika wa mikopo hiyo walitoa shukrani kwa serikali kwa kuwapa fursa ya kujiinua kiuchumi ambapo Yohana Matahe,kwa niaba ya kundi maalumu, ameelezea furaha yake akisema kuwa mikopo hiyo itamwezesha kuboresha maisha yake na ya familia yake.
Mwakilishi wa vijana kutoka kikundi cha Dira Photo Group,Jackson Taranga,amemshukuru Rais Samia kwa kuwaamini vijana na kuwapa mikopo na kuahidi watautumia kwa tija na kurejesha kwa wakati.