Na. Nancy Kivuyo, CHAHWA, DODOMA
Mkutano wa hadhara wa wananchi wa Kata ya Chahwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamefanikiwa kuzindua utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari kwa nguvu zao wenyewe kwa lengo la kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.
Akizungumza na wananchi hao, Diwani wa Kata ya Chahwa, Sospeter Mazengo aliwapongeza wananchi kwa moyo wa utayari na michango katika kujenga shule ya sekondari itakayopunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kupata huduma ya elimu. Baadhi ya wananchi walichanga pesa taslimu pamoja na vifaa vya ujenzi, alisema.
“Watoto wetu wamekua wakiteseka kutembea umbali mrefu kutoka Chahwa hadi Ipala kusoma, ninaamini tutafanikiwa katika hili tuliloazimia kulifanya kama tutaanza kwa nguvu ya pamoja. Inawezekana baadae kupata wadau wakatusaidia kumalizia pale ambapo tutaishia” alisema Diwani Mazengo.
Sambamba na hilo, aliwasisitiza kuwa kupitia maazimio yao waliyojiwekea kufikia mwezi Januari, 2026 madarasa manne yawe yamekamilika na masomo yaanze rasmi.
Kwa upande wake Sarah Mwakyusa, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Chahwa alisema “kata ni yetu, maendeleo ni kwa faida yetu pia, tuwekeze nguvu zetu kwasababu tunaamini kwa kufanya hivyo, serikali itatuona na kutusaidia. Tushiriki ipasavyo katika kuchangia ujenzi huu kwaajili ya maendeleo yetu”.
Aidha, Godfrey Mtundu, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chahwa alieleza kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeendelea kutekelezwa kikamilifu katani hapa kupitia utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali pamoja na uboreshaji wa huduma za kijamii. Alishukuru wananchi kwa jitihada hiyo ya kuunga mkono juhudi za serikali kupitia ujenzi wa shule. “Nawakaribisha wadau mbalimbali mjitokeze kutuunga mkono kwenye ujenzi, tujenge shule yetu kwasababu maendeleo haya ni kwa vizazi vyetu na vya baadae” alimalizia Mtundu.
Naye, John Mtundu alisema “tunasikia raha sana kufanya ujenzi kwaajili ya kuwa na taifa la wasomi la baadae, nitoe rai kwa wananchi wenzangu kuchangia. Mimi naahidi shilingi 50,000 na hapa natanguliza shilingi 20,000. Ninachoweza kusema ni kwamba shule hii itakuwa na manufaa makubwa sana hapa kwetu”.
Mkutano huo uliazimia kwamba mchango wakuendeleza ujenzi wa shule ya sekondari, kila kaya itachangia shilingi 50,000 na mchango utatolewa ndani ya miezi mitano, kila mwananchi atalipia kidogo kidogo shilingi 10,000 kila mwezi. Vilevile, mkutano ulichagua kamati ya viongozi wa ujenzi ambao watakua wawakilishi wa wananchi katika kusimamia utekelezaji wa ujenzi huo.