Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Salome Method kushoto,akiwaonyesha kisima cha maji baadhi ya Wakazi wa Kitongoji cha Dodoma kijiji cha Mterawamwahi kata ya Ligera ambacho kitatarajiwa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 za maji ambalo litahudumia Wakazi wa kitongoji cha Dodoma kijiji cha Mterawamwahi kata ya Ligera Wilayani Namtumbo.
Na Mwandishi Wetu,Namtumbo
WAKAZI zaidi 6,000 wa vijiji vya Kilimasera,Ukiwayuyu,Mtakanini,Mterawamwahi na Matependwe Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kuondokana na kero ya muda mrefu ya huduma ya maji safi na salama.
Ni baada ya Serikali kuipatia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) Wilaya ya Namtumbo Sh.milioni 300,000 kwa ajili ya kutekeleza programu ya uchimbaji wa visima 900/5 kwa kila Jimbo kwa lengo la kupunguza kero ya huduma ya maji katika vijiji hivyo.
Hayo yamesemwa jana na Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilayani Namtumbo Salome Method,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa kisima kirefu cha maji katika Kitongoji cha Dodoma Kijiji cha Mterawamwahi kata ya Ligera.
Alisema,Ruwasa Wilaya ya Namtumbo imeanza kuchimba visima vitano na kazi hiyo ilianza tangu mwezi Oktoba mwaka 2024 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2025.
Method alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa ni uchimbaji wa visima virefu,ujenzi wa vioski vya kuchotea maji,ujenzi wa mfumo wa maji.kuweka matenki ya kuhifadhi maji lita 10,000 kila kijiji,kufunga pampu ya kusukuma maji na kufunga umeme jua(Solar Power).
Kwa mujibu wa Method,kazi zilizofanyika hadi sasa ni uchimbaji wa visima na ununuzi wa vifaa ambapo ujenzi wa vioski vya kuchotea maji unaendelea na kazi hiyo imefikia asilimia zaidi ya 80 ya utekelezaji wake.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uchimbaji wa visima vitano kwa kila jimbo ambavyo vitawezesha kupunguza tatizo kubwa la huduma ya maji kwa baadhi ya vijiji.
Amemshukuru Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mwajuma Waziri, kwa kuikumbuka Wilaya ya Namtumbo kwani miradi hiyo itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutoka asilimia 71 hadi kufikia asilimia 74.
Aidha alisema,Ruwasa Wilaya ya Namtumbo inatekeleza miradi mingine ya maji katika kijiji cha Mchomoro,Msisima-Mnalawi na mradi wa Mgombasi umeanza kutoa huduma katika kijiji kimoja kati ya vijiji viwili.
Diwani wa kata ya Ligera Somebody Mhongo,ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi wa kisima cha maji katika kitongoji cha Dodoma kijiji cha Mterawamwahi ambacho kwa muda mrefu Wananchi wake wanakutumia maji yanayopatikana kwenye mabonde na mito ambayo siyo safi na salama.
Mtendaji wa kijiji cha Mterawamwahi Joseph Haule alisema,changamoto ya maji katika kijiji hicho ni kubwa kwani kuna mabomba mawili tu ya kupampu kwa mkono ambayo hayatoshelezi kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Alieleza kuwa,changamoto hiyo imesababisha kutokea kwa migogoro ya ndoa mara kwa mara pindi wanawake wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji pale wanaume wanapo watuhumu wake zao kutoka nje ya ndoa.
Mkazi wa kitongoji cha Dodoma Lucy Mgala alisema,mradi wa kisima ni mkombozi mkubwa kwani utamaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama na matumizi ya maji kutoka kwenye vyanzo vya asili ambayo yanatumiwa na wanyamapori.
“kwa sasa tunalazimika kwenda kuchota maji mtoni na kwenye mabonde kwa sababu hakuna njia mbadala,hata hivyo wakati wa masika tunaathirika sana kwa kuanguka kutokana na utelezi pindi tunapopanda milima kutoka kuchota maji kwenye mabonde kwa ajli ya matumizi ya familia zetu”alisema.
Mkazi mwingine Kamenya Kawina alisema,wanatembea umbali wa kilometa 1 kila siku kwenda kuchota maji,hali ambayo imesababisha kijiji chao kukosa maendeleo kwa kuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kujikita katika uzalishaji mali.
Ameiomba Serikali kupitia Ruwasa, kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka ili waweze kupata huduma ya maji karibu na makazi yao na wapate muda ya kufanya shughuli mbalimbali za kuwaletea maendeleo.