NJOMBE ,Serikali ya mkoa wa Njombe imefanya kikao cha tathimini ya elimu chenye lengo la kuona mafanikio ,changamoto na kisha kutoka na maazimio ya namna gani sekta hiyo itapiga hatua zaidi na kuwa kinara kitaifa katika mitihani ya ngazi mbalimbali .
Katika kikao hicho ambacho kimeongozwa na mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka ,zimetolewa zawadi kwa wanafunzi,walimu,shule za msingi na sekondari ambazo zimefanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne na sita .
Miongoni mwa shule ambazo zimefanya vyema na kujizoelea zawadi nyingi ni pamoja na Shule ya Sekondari Utalingolo iliyopo kata ya Utalingolo halmashauri ya mji wa Njombe ambayo imetoa wanafunzi wanne walifanya vizuri ambao ni Mario B mkongwa ambae amepata daraja la kwanza la pointi 7,Fredrick A Mtewele pointi 8,Severin A Danda aliyepata daraja kwanza la pointi 8 pamoja na Martin G Msyani mwenye pointi 9 katika matokeo ya kidato cha nne 2024.
Ukiachana na wanafunzi kupata zawadi ,walimu waliyofanya vyema kwenye masomo ya Hesabu na baolojia wametunukiwa ili kuongeza ari ya kufundisha kwa ufanisi wanafunzi
Kufuatia mafanikio hayo Diwani wa kata ya Utalingolo ambae pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete amevujisha siri ya mafanikio hayo kwa shule hiyo changa kuwa ni ushirikiano mkubwa baina ya wazazi ,wanafunzi ,walimu na viongozi wa serikali pamoja na utaratibu uliyoanzishwa 2021 wa kufanya tathimini ya elimu ya kata ili kujua walipopiga hatua na walipoteleza.
Awali afisa elimu mkoa wa Njombe Neras Mulungu alitaja changamoto ya upungufu wa walimu na madawati inavyokwamisha jitihada za mkoa huo kufikia kusudio lake la kuwa kinara kitaifa katika mitihani ya ngazi zote huku pia akieleza jitihada zinazochukuliwa ikiwemo kuajiri walimu wa kujitolea na kufunga mifumo ya tehama mashuleni ili kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja kupitia mfumo wa computer.
Baada ya kupokea mapendekezo ya wadau ndipo mwenyekiti wa kikao hicho ambae ni mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda anasisitiza kuanza utaratibu wa tathimini za elimu kwa kila kata kama ilivyo kwa kata ya utalingolo ambayo inakua kwa kasi kitaaluma na kisha kuonya tabia za ukatili na ubakaji kwa watoto na wanafunzi ambao umekua ukitokea mara kwa mara mkoani humo.


