Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imepanga kutoa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa vijana 5040 kupitia mradi wa Timiza Malengo.
Mradi huu kwa upande wa VETA unatekelezwa katika mikoa 6 na Halmashauri 18 za mikoa ya Ruvuma, Njombe, Tabora, Lindi, Mara na Tanga na umepangwa kukamilika ifikapo Desemba 2025.
Akizungumza jana Wilayani Ruangwa wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa Timiza Malengo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa(MB), amesema kuwa mradi wa Timiza Malengo unalenga kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa vijana balehe wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 24 walio mashuleni na nje ya mfumo wa elimu kwa kuwapatia Elimu ya Ufundi stadi na kuwajengea uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi.
Amesema kuwa serikali kupitia miradi mbalimbali imefanikiwa katika utoaji wa mafunzo na stadi za maisha kwa vijana kupitia taasisi kama vile VETA na Vyuo vya Elimu ya Amali.
“Mradi wa Timiza Malengo kwa awamu ya tatu umelenga kuwafikia na vijana balehe wa kike na kuwapa Elimu ya Ufundi stadi kupitia vyuo vya VETA, kuwaunganisha na taasisi za ufundi hususan VETA, pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo nafuu ikiwemo mikopo ya 10% inayoratibiwa na serikali kupitia wizara ya TAMISEMI.”amesema
Amesema, Serikali inaendelea na mipango ya kisera na kimuundo kuhakikisha hadi ifikapo 2030 Tanzania iwe imefanikiwa kufikia 0.3% katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya, kuzuia vifo vitokanavyo na VVU/UKIMWI pamoja na unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na maambukizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi Stadi VETA Dkt. Addallah Ngodu akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, amesema VETA kupitia mradi wa Timiza Malengo umepanga kuwafikia wanufaika 5,040 walio hatarini kupata maambukizi ya Ukimwi katika Halmashauri 18 kutoka mikoa 6 ya Ruvuma, Njombe, Tabora, Lindi na Mara ambapo vijana katika mikoa hiyo watapata elimu katika fani mbalimbali.
“Jumla ya wanufaika 3142 wamepatikana kwa Mkoa wa Ruvuma na Njombe tayari kwa kuanza mafunzo tarehe 24 Februari, 2025 katika fani 12 za mafunzo ya Ufundi Stadi.” amesema Mgodu.
Aidha, Mkoa wa Lindi jumla ya wanufaika 1,233 wamepatikana kujiunga na Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kati yao wanao toka Lindi Manispaa ni 562 na Wilaya ya Ruangwa ni 671.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Catherine Joachim ameishukuru serikali kwa kukubali kutekeleza mradi huu kwakua utawafikia wasichana balehe na wanawake vijana ambao ni kundi lililopo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU.