
Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ukimo kata ya Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wakichota maji baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)kufikisha maji ya bomba katika kijiji hicho ambacho kwa muda mrefu hawakuwa na huduma ya maji ya Bomba
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
WAKAZI wa kijiji cha Ukimo kata ya Mbangamao Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwajengea mradi wa maji ya Bomba utakaomaliza adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Wamehaidi kulinda mradi huo ili uendelee kuwanufaisha wao na kizazi kijacho, kutokana na changamoto kubwa waliopitia ya kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Mkazi wa kijiji cha Ukimo Regina Ndunguru,amewapongeza wataalam wa Ruwasa ngazi ya Wilaya na Mkoa kwa kuanza kutekeleza mradi huo kwani utawaondolea adha ya muda mrefu ya kuchota maji kwenye vidimbwi.
Alisema mradi huo ni neema kubwa kwao,kwani walikuwa wanachota maji kwenye vyanzo ambavyo maji yake siyo safi na salama na inawalazimu kwenda umbali mrefu na kuamka usiku kufuata maji,hivyo kuhatarisha maisha kwa kugongwa na nyoka na ndoa zao kuwa mashakani na utawapunguzia gharama ya maisha ya kununua maji ndoo moja ya lita 20 kwa bei ya Sh.1,000.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ukimo Kanuni Mbunda,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za mradi wa maji, kwani wanapata changamoto kubwa katika utendaji wa majukumu yao hasa pale wanapolazimika kubadili ratiba za masomo ili watoto wakatafuta maji kwanza kabla ya kuingia darasani.
Alisema,kwa kuwa maji yamefika hadi shuleni yatawasaidia Wanafunzi kwa kufanya usafi na kuepukana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu kwani Wanafunzi wataweza kujisaidia na kunawa mikono kwa usahihi.
“maji ni muhimu kwani yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kirahisi kwa sababu wanahitaji kufanya usafi kwa wakati kabla ya kuingia darasani,kuna wakati tunachelewa kuingia darasani hadi wanafunzi wafanye usafi”alisema Mwalimu Mbunda.
Hata hivyo alisema,pamoja na changamoto za maji walipambana na mazingira yaliyopo kwa kufuata maji kwenye vyanzo vingine vilivyopo,kupanga ratiba za masomo vizuri hali iliyowezesha Shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma
Naye Mwanafunzi wa Shule hiyo Upendo Mbunda alisema,awali walikuwa wanachelewa kufika shuleni kwa sababu kabla ya walitakiwa kwanza kwenda mtoni kuchota maji kwa ajili ya usafi nyumbani ndipo waende shule jambo lililochangia kushukwa kwa taaluma kwa Wanafunzi.
Alisema,sasa hawapotezi muda wa kwenda mtoni kuchota maji kwani yanapatikana kwenye makazi hayo,hivyo ni rahisi kila asubuhi wanapoamka wanafanya shughuli za nyumbani na kuwahi vipindi dasarani.
Pia alisema,suala la usafi wa mazingira lilikuwa jambo gumu kutokana na kukosa maji ya uhakika,lakini baada ya kupata mradi wa maji ya bomba watafanya vitu vingi kwa wakati mmoja bila kuathiri ratiba za masomo.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(Ruwasa)Wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alitaja gharama za mradi huo ni Sh.milioni 30 zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maji.
Sinkala alisema,mradi utakapokamilika utasaidia sana kupunguza magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na matumizi ya maji ya visima vya asili ambayo siyo safi na salama na kutatua changamoto ya huduma ya maji safi kwa wakazi wa kijiji hicho.
Alisema,chanzo cha mradi huo ni chemchem ya asili iliyoboreshwa na kazi zitakazopangwa kutekelezwa ni kujenga matenki ya kuhifadhi maji,kujenga vituo vya kuchota maji na kulaza mabomba kutoka kwenye chanzo hadi kwa watumiaji(Wananchi).
MWISHO.