Na Mwandishi wetu, Mirerani
WEZI wamevunja stoo ya kuhifadhi vyakula kwenye kituo cha watoto yatima, wenye uhitaji maalum na waliokuwa kwenye mazingira magumu cha Light In Africa kilichopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kuiba vyakula vyenye thamani ya Sh468,000.
Mmoja kati ya walezi wa kituo hicho, Jasmin Kimaro akizungumza na waandishi wa habari amesema wizi huo umetokea usiku wa Februari 9 mwaka 2025.
Kimaro ametaja vyakula vilivyoibiwa ni mchele kilo 50, mafuta ya kula lita 10, sabuni ya kufulia ndoo mbili ndogo, pipi pakiti mbili za lol pop, maharage kilo 35, ndizi mbivu vichane vitatu, soda katoni mbili na ndoo ndogo tupu waliyotumia kubebea baadhi ya vitu.
“Tumeshatoa taarifa polisi juu ya wizi huo kwani siku hiyo tuliamka asubuhi na kubaini mlango wa eneo la kuhifadhi vyakula upo wazi umevunjwa na vitu hivyo kuibiwa,” amesema Kimaro.
Ameeleza kwamba pamoja na kuwa na mlinzi kwenye kituo hicho ila waliibiwa kwani alikuwepo siku hiyo ila alipitiwa na usingizi na kutokea tukio hilo.
Mlezi mwingine wa kituo hicho, Mariam Mkali amesema wamesikitishwa na kitendo hicho cha watu kuingia katika kituo hicho na kuiba vyakula.
Mkali amesema siku ya tukio hilo watoto walichelewa kula asubuhi kwani vyakula ambavyo walitarajia kuwapikia vilikuwa vimeibiwa na wezi.
Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Ahmed Makarani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la wizi kwenye kituo hicho cha watoto.
Kamanda Makarani amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini waliohusika na wizi huo katika kituo hicho cha watoto.
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Sokoto Mbuya amesema kwamba amesikitishwa na kitendo cha wizi kilichotokea kwenye kituo hicho cha watoto.
Sokota amesema wezi hao wanapaswa kutambua kuwa kituo cha watoto yatima, wasiojiweza na waliokuwa wanaoishi kwenye mazingira magumu ni sawa na nyumba ya ibada hivyo inapaswa iheshimiwe.