Mchumi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma , Francis Kaunda ameupongeza mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) pamoja na bodi ya mikopo ya vyuo vya elimu ya juu nchini (HELSB),kwa kutekeleza adhma ya serikali ya kuwapa mikopo ya asilimia 100 watoto wanaotoka kaya maskini kwa ya kuendelea na elimu ya juu.
Kaunda amesema hayo leo Leo Februari 14 2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Dodoma mjini,wakati akifunga maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya mikopo yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere square jijini hapa.
Akiwa katika Banda la TASAF,Kaunda amesema umuhimu wa elimu upo kwa kila mmoja,hivyo ushirikiano wa HELSB na TASAF unastahili kupongezwa kwa sababu umeonyesha namna bodi hiyo Samia inavyotenda haki.
“Nawapongeza TASAF na HELSB kwa ushirikiano mnaofanya mmetimiza malengo ya serikali ya kutaka kila mmoja apate elimu,”amesema Kaunda.
Naye mnufaika wa mfuko wa maendeleo (TASAF) Lightness Mwasanu ameeleza namna ruzuku inavyotolewa na kunufaisha familia zinazoishi katika mazingira masikini.
Mwasanu amesema TASAF imekuwa na mchango mkubwa sana kwa Kaya maskini kutokana na kwamba wengi wa wanafunzi waliotoka kaya maskini wameendelea na masomo ya elimu ya juu.
Amesema anaishukuru serikali kupitia mfuko wa TASAF kwa sababu umekuwa chachu ya kuibua wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali.
Amesema TASAF imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanaotoka kaya maskini wanatimiza ndoto zao katika suala zima la elimu.