Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Bi. Stella Tullo,akizungumza na mawakili , wa kujitegemea katika kikao kazi kilichofanyika Februari 12, 2025, kwenye ofisi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake, Bi. Tullo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha na kuwashauri wananchi kutumia njia za usuluhushi kumaliza migogoro ya ardhi,kwani usuluhishi unajenga zaidi amani na upendo ndani ya jamii.
Dar-Es-Salaam
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini, Bi. Stella Tullo, amesisitiza umuhimu wa mashauri kumalizika kwa wakati na kwa Haki ili kuhakikisha wananchi wanapata haki za umiliki wa Ardhi zao kwa haraka kwani Ardhi ni rasilimali Muhimu ya kuwawezesha kuendesha Shughulli za kujipatia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Bi. Tullo ameyasema hayo Februari 12, 2025, alipokutana na mawakili wa kujitegemea katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ofisi za Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Bi.Tullo amewataka mawakili na wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi jijini Dar es Salaam kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia muda wa mashauri ili kuharakisha uamuzi wa kesi. Ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha mashauri yote yanamalizika ndani ya muda mfupi, huku akisisitiza kuwa mashauri yaliyodumu Barazani zaidi ya miaka miwili (backlog cases) yanapaswa kupewa kipaumbele zaidi yamalizike kwa haki na kwa haraka ili kupunguza msongamano wa kesi.
Aidha, Bi.Tullo amewapongeza wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wao mzuri na wadau wa utoaji haki. Ameeleza kuridhishwa na juhudi zao za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za mashauri ya ardhi, pamoja na ushiriki wao wa dhati katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini.
“Tumeona maendeleo chanya kutokana na ushirikiano wenu na mihimili mingine ya utoaji haki. Ni muhimu tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati,” alisema Bi.Tullo.
Kwa upande wake, Wakili Geofrey Luhanji, akizungumza kwa niaba ya mawakili wa kujitegemea, amemshukuru Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kwa kuitisha kikao hicho. Alisema kuwa kikao hicho kimewapa fursa ya kujadili changamoto na kupata suluhisho la pamoja kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.
“Tunamshukuru Bi.Tullo kwa kutupa nafasi ya kushiriki kwenye kikao hiki muhimu.Tumepata fursa ya kujadili masuala muhimu ambayo yameimarisha mahusiano yetu na kutukumbusha wajibu wetu wa kuhakikisha mashauri yote yanamalizika kwa wakati,” alisema Wakili Luhanji.
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba nchini yamekuwa na jukumu muhimu katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa wakati na kwa haki. Hatua hii ya Msajili wa Mabaraza ya Ardhi inatarajiwa kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi nchini kote.
Sehemu ya mawakili wa kujitegemea wakifuatilia kwa makini maelezo ya Bi. Tullo wakati wa kikao kazi hicho. Kikao ambacho kimewaleta pamoja wadau muhimu wa sekta ya ardhi kujadili mbinu za utoaji wa huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa haki na kwa wakati.
Mmoja wa washiriki akichangia hoja wakati wa kikao kazi, akieleza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa mashauri ya ardhi na namna ya kuzitatua kwa kushirikiana na mabaraza ya Ardhi ya Wilaya nchini.