Na.Mwandishi Wetu
SERIKALI imerekebisha Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za Mwaka 2019 na kutoa kanuni mpya za mwaka 2023 na kutangazwa katika gazeti la serikali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni nchini.
Marekebisho hayo yamesaidia kuongezeka kwa idadi ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Zanzibar kutoka maduka 4 yenye matawi 11 hadi maduka 15 yenye matawi 35.
Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande amesema hay oleo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni Ussi Salum Pondeza lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.
Katika swali lake ametaka kujua Serikali imechukua hatua gani za kuhakikisha huduma za kubadilisha fedha zinapatikana karibu na Hoteli za kitalii Zanzibar.
Akijibu swali hilo Chande amesema hatua hiyo ni moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali kuwezesha upatikanaji wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni kwa urahisi nchini ikiwemo Zanzibar.
Amesema katika utoaji wa leseni, kanuni zimeweka madaraja matatu ya maduka ambayo ni daraja A,B na C na kupunguza mtaji unaohitajika katika kuanzisha maduka hayo.
Amesema mabadiliko hayo yametoa fursa kwa hoteli zenye hadhi ya nyota tatu au zaidi kuomba leseni za kufanya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni kupitia dirisha la daraja C.
Katika swali la nyongeza Mbunge Mtaturu ametaka kujua kanuni mpya zimesaidia kwa kiasi gani uendeshwaji wa maduka ya fedha za kigeni lakini pia mwaka 2017/2018 kulikuwa na utaratibu wa kusitisha leseni za wafaynyabiashara wanaofanya biashara hiyo katika mikoa ya Arusha na Dar es salaam je maduka yalikuwa mangapi na sasa hali ikoje ili shughuli ziendelee kama kawaida kwa wafanyabiashara hao.
Akijibu maswali hayo Chande amesema sheria imesaidia kwa kiasi kikubwa sana na ndio maana kuna ongezeko la maduka na hiyo ni kwa sababu ya punguzo lililopo kwenye mtaji ambayo imegaiwa katika madaraja matatu.
“Daraja A gharama ya mtaji ni Bilioni 1,daraja B Milioni 500 na daraja C ni Milioni 200 hivyo imeongeza idadi ya huduma ya maduka hayo,swali lake la pili naomba nijibu kuwa ni kweli mwaka alioutaja ilitokea kufutwa leseni kwa baadhi ya maduka na idadi yake ilikuwa maduka 65 na kwa bahati nzuri maduka 61 yamerejeshewa leseni na huduma inaendelea,”.amesema