Na John Walter -Babati
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati, Filbert Mdaki, ametoa onyo kali kwa wale wanaotembea kuwashawishi wajumbe ili wawapigie kura kwenye nafasi za Ubunge na Udiwani kabla ya muda rasmi wa mchakato wa uchaguzi kufika.
Mdaki ametoa kauli hiyo wakati wa sherehe za miaka 48 ya CCM katika Kata ya Mwada, ambapo sherehe hizo ziliambatana na matembezi maalum ya kupongeza mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, ambao uliwapitisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais kwa Tanzania Bara na Dkt. Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar.
Katibu huyo amesema ana taarifa za watu ambao tayari wameanza kampeni za chinichini kwa lengo la kushawishi wajumbe, akisisitiza kuwa tabia hiyo inakiuka utaratibu wa chama na inaweza kuwakosesha sifa wagombea husika pindi mchakato rasmi utakapofika.
“Kwa uchaguzi wa mwaka huu, hata wagombea wawe 1000, watakaopigiwa kura ni watatu tu kwenye kura za maoni,” alisema Mdaki, akiwataka wanaotaka kugombea kusubiri muda mwafaka badala ya kufanya kampeni za mapema.
Kwa sasa, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ni Daniel Sillo, na madiwani waliopo wataendelea kuhudumu hadi muda wa uchaguzi utakapowadia rasmi.
Mdaki amesisitiza kuwa CCM ina utaratibu wake wa kuchagua wagombea na kwamba maadili ya chama yanapaswa kuheshimiwa.
Onyo hili linakuja wakati ambapo harakati za kisiasa zinaanza kushika kasi kuelekea uchaguzi ujao, huku chama kikipanga kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa uwazi na haki.