WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , Mohamed Mchengerwa,akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu kati ya halmashauri 10 na benki mitatu,hafla iliyofanyika jijini Dodoma
…….
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa,ametoa onyo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi endapo itabainika kuwa vikundi hewa katika maeneo yao vilivyonufaika kupitia mikopo ya asilimia 10, watawajibishwa.
Waziri Mchengerwa ametoa onyo hilo jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulamavu kati ya halmashauri 10 na benki mitatu.
Amewataka Mkuu wa Mkoa , Wilaya na Wakurugenzi wafuatilie kwakuwa hataki kusikia vikundi hewa.
“Nawambia wazi kabisa, tumefika hapa kwasababu kuna watumishi wasio waaminifu ambao walitafuna fedha hizi kwa kukopeshana wenyewe na hawakuwa na sifa ya kupokea mikopo hii.”amesema Mchengerwa
Aidha Mchengerwa amesisitiza kuwa uadilifu kwenye fedha hizo na kuwataka wafuatilie vikundi vyote na kuvijua na asisikie vikundi hewa.
“Fedha hizi ni za moto wajibu wetu ni kumsaidia Rais fedha hizi zisiende kuchezewa, naelekeza kikundi hewa kitakachobainika eneo lolote viongozi wa eneo hilo mtapaswa kuwajibika, tumieni vyombo mnavyosimamia kwenye mikoa na wilaya kuhakikisha hakuna vikundi hewa, fedha zisimamiwe na kurejeshwa.”amesisitiza
Hata hivyo amesema vikundi vyote vinavyopokea mikopo hiyo vinatakiwa kufanya shughuli za uzalishaji na kurejesha fedha kulingana na mipango ya marejesho.
“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi tumekubaliana jukumu la usimamizi wa fedha hizi ni la kila mmoja wet una wakati tunamshauri Rais sisi Wizara tulimhakikishia kuanzia kwangu kwamba iwapo kutakuwa na kulegalega kukote mimi na wasaidizi wangu tutalazimika kuwajibika.”
Amesema Benki ya NMB itafanya kazi kwenye halmashauri za wilaya za Bumbuli, Itilima, Newala, Manispaa ya Songea, Jiji la Dodoma huku benki ya CRDB itafanya kazi Wilaya za Nkasi, Mji wa Mbulu, Manispaa ya Kigoma na Jiji la Dar es salaam.
Hata hivyo, amesema Benki ya Biashara ya Uchumi itafanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
“Zaidi ya Sh.Bilioni 234 zinakusudiwa kupelekwa kwa wananchi kwa njia mbili za utoaji mikopo hiyo ambazo ni kupitia Benki kwa Halmashauri 10 na mikopo iliyoboreshwa kwenye Halmashauri 174.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Adolf Ndunguru amesema kuwa kusainiwa mikataba hiyo ni mwanzo wa mapinduzi ya kuhakikisha mikopo hiyo ya asilimia 10 inakuwa na tija tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.