Na Hellen Mtereko,Mwanza
Kata ya Nyegezi iliyoko Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza imeendelea kutekeleza vizuri upatikanaji wa huduma ya chakula shuleni hatua inayosaidia kuchochea ubora na ufaulu kwa wanafunzi.
Hayo yamebainishwa Feburuari 04, 2024 katika kikao cha kamati ya lishe ngazi ya Wilaya robo ya pili mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mtendaji wa Kata ya Nyegezi, Shabani Mpuya alisema suala la lishe kwenye shule za sekondari na msingi wazazi wamekuwa na mwitikio mzuri wa kuchangia chakula shuleni kwa wakati.
“Miongoni mwa shule ambazo watoto wanapata huduma ya chakula ni shule mpya ya msingi swira na shule ya sekondari Nyaburogoya wazazi wanajitoa vizuri kwani tumekubaliana kuanzia darasa la tatu hadi la tano wanachangia shilingi 500 kila siku na darasa la sita hadi la saba ni 1000 na wazazi wanatoa fedha hizo kwa wakati”,
Aidha, amesema kuwa endapo kunachangamoto katika shule ambazo ziko kwenye kata nyingine waende wajifunze kwenye Kata ya Nyegezi.
Kwaupande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dkt. Furaha Mwakafwila alisema katika kikao hicho wameazimia kuhakikisha watoto wanapata chakula mashuleni kwakuendelea kuihamasisha jamii umuhimu wa watoto kula shuleni.
Alisema wazazi wanapaswa watambue umuhimu wa watoto wao kula chakula shuleni ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Akizungumza nje ya kikao hicho Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala ambae alikuwa anaongoza kikao hicho alisema takwimu zinaonesha kwaupande wa shule zamsingi suala la lishe liko asilimia 49 huku sekondari ikiwa ni asilimia 53.
Alisema wazazi wanahimizwa sana kwenye uchangiaji wa chakula mashuleni,pamoja na kuwepo kwa mwitikio mdogo hususani katika shule zilizoko kwenye kata ya Igogo na Isamilo kuna kata ambazo zinafanya vizuri ikiwemo kata ya Nyegezi.
“Tumejipanga kufanya vikao na kamati za shule ili tuweze kukubaliana mbinu za kuendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa chakula mashuleni ili tuendelee kupanda angalau kwenye shule za msingi tufike asilimia 80 na sekondari asilimia 90”, alisema Salala