Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Desderius Haule,akizungumza jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri eneo la Kihamili,katikati Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Bahati Mbele na kulia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Pascal Ndunguru.
Picha no 942 Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Desderius Haule(hayupo pichani) wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri eneo la Kihamili jana.
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma,limewasimamisha kazi Watendaji saba wa vijiji kwa upotevu wa Sh.milioni 28,236,400 kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Shilingi milioni 28 ambazo walikusanya kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato vya Halmashauri kupitia mashine za POS na kushindwa kupeleka Benki fedha.
Maazimio ya kuwasimamisha kazi Watumishi hao yametolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Desderiue Haule mara baada ya Baraza kugeuka kuwa kamati ili kuwajadili Watumishi hao baada ya kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Alisema,Halmashauri iliunda Tume maalum ya kuchunguza upoteza huo na imebaini watendaji wametumia fedha hizo bila kufuata kanuni,taratibu na sheria za kuomba idhini ya kuhamisha fedha au kubadilisha matumizi kutoka kifungu kimoja kwenda kingine na kushindwa kufanya mrejesho katika Ofisi ya Mweka Hazina.
“Watendaji hao baada ya kufikishwa kwenye kamati ya maadili,Waheshimiwa Madiwani wameunga mkono hoja na mapendekezo ya tume ya uchunguzi na timu iliyoundwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri juu ya kuwasimamisha kazi na wanatakiwa kurudisha fedha hizo”alisema Haule.
Aidha,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Tume iliyochunguza suala la nidhamu kwa Watumishi hao ambapo ameagiza kuwasimamia ili waweze kurejesha fedha walizochukua.
Katika hatua nyingine Haule alisema,Baraza la Madiwani limemsimamisha Diwani wa Kata ya Mapera Betram Komba,kutohudhuria vikao vitatu baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka maadili ya kikanuni kwenye vikao,kutoa lugha isiyokuwa staa na kufanya vurugu kwenye kikao.
Haule,amewapongeza Watumishi na Madiwani kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuibua vyanzo vipya na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani hali iliyowezesha Halmashauri hiyo kuwa kinara wa kukusanya mapato kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma.
Kwa upande wake Afisa Rasilimali Watu wa Halmashauri hiyo Festo Mwangalika amewataja Watendaji hao na fedha walizoshindwa kupeleka benki ni Festho Komba(Sh.milioni 7,527,100) Mwajuma Matily (Sh.580,000) na Shaban Mkongo( Sh.582,000), Fotnatus Ngongi(2,626,000)Keneth Moyo(10,448,000)Sotely Kawhili(2,734,300) na Gaston Mbunda(Sh.3,739,000).
“Halmashauri imewasimamisha kazi kwanza ili wasiendelee na majukumu yao wakati uchunguzi wa suala lao unaendelea,lakini baada ya kuitwa kwenye kamati ya maadili baadhi yao wameanza kurejesha fedha walizochukua”alisema.
Mwangalika alisema,kosa la Watumishi hao ni kukusanya fedha bila kuzipeleka Benki jambo ambalo ni kinyume na sheria za Mamlaka ya Serikali ya mwaka 2009 na wamepewa muda wa miezi sita kurejesha fedha hizo na taratibu nyingine zilizopendekezwa na kamati zitatekelezwa juu yao.