TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imefanikiwa kurejesha matumaini ya Meshack Simeo, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Namonge wilayani Bukombe mwenye ndoto ya kuwa daktari.
Hatua hiyo inakuja baada ya wanasheria hao kutembelea shule hiyo na kutoa elimu ya sheria ambapo Meshack alitumia fursa hiyo kuelezea changamoto za kifamilia ambazo zilitaka kukatisha ndoto zake.
Akizungumza baada ya kupata msaada Meshack amepongeza kampeni ya msaada wa kisheria kwani kijijini hapo kumekuwa na shida kubwa ya wanafunzi wengi kukatisha masomo kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Katika familia yetu sisi tupo watoto kumi, tunaishi na mama yetu lakini baba hayupo, na mama hana uwezo wa kutuhudumia kwa hiyo tunapata mahitaji machache na tukiwa shuleni tunajipambania wenyewe.”Aliendelea kusema
“Hata mimi mwenyewe hapa fedha zinakosekana kwa ajili ya fedha za masomo, nilikuwa na ndoto za kuwa daktari lakini ni gharama kubwa, nikaamua nisitishe sielewi hata nifanyeje kwa sababu ya changamoto za kimaisha”.
Amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia umerejesha matumaini yake kwani watamsaidia kutoa muongozo ili baba yake atimize wajibu wake kwa kutoa huduma zote kwa familia aweze kutimiza ndoto yake.
Mama yake Meshack, Marietha Mateo amesema changamoto ilianza baada ya mtoto wao wa kiume kufariki ndipo mme wake (baba Meshack) alipoamua kutelekeza familia kwa madai ya kuhofia usalama wake.
Amesema mme wake kwa sasa hatoi huduma kwa watoto na imesababisha kaka zake Meshack kushindwa kuendelea na maasomo baada ya kuhitimu kidato cha nne na hivo msaada wa kisheria wa Samia utasaidia kutatua tatizo.
Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) Majid Kangile aliahidi watawasiliana na baba yake Meshak kwa hatua zaidi ili aweze kuwajibika kutoa huduma stahiki kwa watoto wake akiwemo Meshack.
Amewataka wanandoa kufuata taratibu za kuvunja ndoa badala ya kutelekeza familia na watoto ili kuepuka kuharibu ndoto za watoto kutokana na migogoro ya kifamilia.
Amesema hakuna mwanandoa mmoja mwenye haki na mali zote za familia na hivo wanapotengana ni lazima hatua za kugawana mali zifuatwe kwa kuzingatia maslahi ya watoto badala ya mtu mmoja kumiliki ama kuuza mali zote.