Kaimu Mkurgenzi wa Manispaa ya Ilemela,Egidy Teulas, akiwasilisha kwa madiwani (hawapo pichani), taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25, leo.Katikati ni Meya wa Manispaa hiyo, Renatus Mulunga na kushoto,Naibu Meya, Manusura Said Lusigaliye.
NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela, hadi kufikia Disema 31,mwaka jana, imekusanya zaidi ya bilioni 7 za mapato ya ndani sawa na asilimia 47,ya lengo la kukusanya sh.bilioni 14.7 mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Egidy Teulas,leo wakati akitoa taarifa ya robo ya pili (Oktoba-Disemba) ya mwaka wa fedha 2024/25,akisema kiasi hicho ni sawa na asilimi 93.8,ya lengo la nusu mwaka.
Amesema katika robo ya pili ya mwaka huu wa fedha, zaidi ya milioni 270.9 za mapato ya ndani,zilielekezwa katika miradi ya maendeleo na kati ya fedha hizo,milioni 70 za ununuzi wa eneo la ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Nyasaka.
Kwa mujibu wa Taulas sh. milioni 25,zilishaji vyumba viwili vya madarasa shule ya msingi Magaka, milioni 23.9 zilitumika kununua viti na meza 350 kwa shule za sekondari,milioni 23.0 za madawati 325 kwa shule za msingi awamu ya kwanza,milioni 36 za ujenzi wa vyoo vya shule za sekondari Bujingwa na Ibinza.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema,halmashauri hiyo iliendelea kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ambapo imefikia hatua mbalimbali kwa gharama ya sh.bilioni 2.4 za mapato ya ndani.
Amesema sh.milioni 300 zilitumika kununua vifaa tiba vya Hospitali ya Wilaya ya Ilemela,huku sh.milioni 239 zikitumika kukamilisha hospitali hiyo ya wilaya, uenzi wa bweni shule ya sekondari Wavulana ya Bwiru uligharimu milioni 130.
Pia , ujenzi wa bwalo la shule ya sekondari Sangabuye uligharimu zaidi ya milioni 113.3,ununuzi wa vifaa tiba vya zahanati zilitumika milioni 100,huku sh.milioni 83.7 za Mfuko wa Jimbo zikitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Tunamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,kwa kuendelea kutoa fedha kwa za miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Ilemela ambapo imeendelea kutekeleza miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya sh.bilioni 2.5 zilitolewa na serikali kuu,”amesema.
Aidha, halmashauri hiyo katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka jana,ilishika nafasi ya tisa kitaifa, nafasi ya tatu kikanda na mkoa nafasi ya kwanza.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela,Renatus Mulunga,amesema kazi ya ukusanyaji mapato ni la ushirikiano na kuwaomba madiwani kuendelea kushirikiana na watendaji katika suala hilo.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anazofanya na fedha nyingi za maendeleo alizotuletea Ilemela na zinaendelea kuja.Raia yangu tuendelee kukusanya mapato na halmashauri isiyokusanya mapato maendeleo yake yatakuwa duni pia, suala la maendeleo si la CCM,CUF bali la wananchi wote,”amesema.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela,Mariam Msengi,amewapongeza madiwani hao kwa kazi kubwa waliyofanya mwaka jana na kuwataka wakasimamie utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato.
“Kazi iendelee na tweni tukasimamie miradi ya maendeleo na thamani ya fedha hizo ionekane kwa wananchi na tukasimamie vema ukusanyaji wa mapato na watumishi wetu ili wananchi wapate huduma bora na stahiki,”amesema.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Diwani wa Pasiansi, Rosemary Mayunga, amesema,taarifa hiyo ni nzuri na imesheni kila upande lakini akasisitiza elimu awali ipewe kipaumbele zaidi.