Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi (Mb) akijibu swali Bungeni leo tarehe 31 Januari, 2025, jijini Dodoma.
Na; Mwandishi Wetu – DODOMA
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema kuwa Mifuko ya hifadhi ya jamii imeendelea kufanya maboresho zaidi katika matumizi ya TEHAMA ili kutoa huduma kwa urahisi kwa wanachama wake na wastaafu.
Mhe.Katambi ameyasema hayo hii leo Januari 31, 2025 Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Tecla Ungele ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka huduma za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika ngazi za wilaya na tarafa ili kuwaondolea usumbufu wastaafu kwenda kuhakiki mkoani.
Akijibu swali hilo, Mhe. Patrobas Katambi amesema Wastaafu kwa sasa wanaweza kujihakiki kupitia simu janja (Smartphone) kupitia programu ya kidijitali (Online Portal) bila kufika katika ofisi za Mifuko.
Ameongeza kuwa, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa wanachama, wastaafu na wadau wote wanao husika katika mtiririko wa mafao kuhusu huduma zinazotolewa kupitia TEHAMA.
Kadhalika, Katambi amesema uhakiki wa uanachama unafanyika katika ofisi za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zilizoko mikoani na wilayani na ukusanyaji wa taarifa ni shirikishi ngazi zote ikiwemo ngazi ya Tarafa, Wilaya na Mkoa.