Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda, akifungua Mkutano wa wadau wa zao la choroko na mfumo wa stakabadhi za ghala uliofanyika mkoani humo
Meneja wa Mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko (COPRA),Irene Mlola akitoa ufafanuzi wa mfumo wa stakabhi za ghala kwa wadau wa zao la choroko Mkoani Mwanza
Baadhi ya wakulima wa zao la choroko wakiwa kwenye mkutano wa kujadili mfumo wa stakabadhi za ghala.
Wadau zao la choroko wakiwa kwenye mkutano
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefungua mkutano wa wadau wa zao la Choroko wenye lengo la kuelimishana umuhimu wa matumizi ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Akizungumza na wadau hao Jana Januari 29, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo kwenye Ofisi ya mkuu wa mkoa, Mtanda amesema mfumo huo ni muhimu kwani utakuwa ni mkombozi kwa wakulima kuweza kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kuepukana na baadhi ya vishoka wanaofaidika kwa ulaghai.
Mhe. Mtanda amebainisha huu ni mpango wa Serikali wenye nia njema ya kuhakikisha mkulima ananufaika na shughuli zake za shambani hivyo mazao ya jamii ya mikunde ambayo awali ilikuwa kama yamesahaulika sasa yanaenda kuwa na tija kwa wakukima.
“Serikali imeunda Mamlaka ya udhibiti wa nafaka na mazao mchanganyiko (COPRA) kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri wa mazao hayo kuanzia kilimo bora kitakacholeta uvunaji bora pia na bei nzuri kupitia mfumo wa Stakabadhi Ghalani”,ameeleza Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola amesema katika mfumo huo wataanza na mazao ya makundi matano ambayo ni nafaka ukiwemo mpunga na Mahindi,mbegu za mafuta ikijumuisha alizeti,michikichi, na ufuta,jamii ya bustani ni pamoja na maua na mbogamboga huku jamii ya mikunde itajumuisha choroko,mbaazi,dengu na soya na jamii ya mizizi ni viazi,mihogo na magimbi.
Aidha, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Innocent Keya akizungumzia uzalishaji wa zao la Choroko mkoani Mwanza amebainisha kwa msimu wa mwaka 2023 hadi 2024 Mkoa ulivuna tani 16,862.
Kwau pande wake Mtaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Agustino Nduganda amesema msimu huu wa Masika Mkoa wa Mwanza utakuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani,wilaya za Kwimba,Magu,Misungwi na Sengerema zinazolima kwa wingi Choroko zitakuwa na mvua za milimita 350 hadi 400 ni vizuri wakulima wafahamu na kuzingatia taarifa hii ili wajipange vizuri.
Katika kikao hicho wadau wa mkutano huo ambao ni wenyeviti wa Halmashauri,wakuu wa wilaya wakulima na wasambazaji wameitaka COPRA kuendelea kuufanyia utafiti mzuri mfumo wa Stakabadhi Ghalani kabla haujaanza kutumika rasmi mkoani Mwanza.