Mafundi wakiendelea na ujenzi wa mitaro ya kupitisha maji kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kihamili-Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga eneo la Kigonsera ambayo inajengwa ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirisha wa bidhaa na mazao ya kilimo.
Muonekano wa Barabara mpya Kihamili-Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma inayojengwa kwa kiwango cha lami na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini Tanzania(TARURA).
Na Mwandishi Wetu,Mbinga
WAKALA wa Barabara za vijijini na mijini Tanzania(TARURA)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,umetenga zaidi ya Sh.milioni 468 ili kuendelea na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kihamili-Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kiwango cha lami.
Ujenzi wa Barabara hiyo unalenga kuwaondolea Wananchi adha ya usafiri wanapokwenda kupata matibabu kwenye Hospitali hiyo,kurahisisha huduma ya kusafirisha mazao na kukuza kipato cha Mwananchi mmoja mmoja,wilaya ya Mbinga na Taifa kwa ujumla.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga Oscar Mussa amesema,Barabara hiyo inajengwa kwa awamu na ina urefu wa kilometa 3.4 na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa mita 750.
Aidha Mussa, ametaja kazi nyingine zilizotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilometa 3.5 kuelekea makazi mapya ya viongozi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga.
Alisema,licha ya kurahisisha usafiri kwa wananchi watakaokwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Halmashauri,Barabara hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA)kwenda na kurudi chuoni na kuboresha Barabara katika eneo la Kihamili ambalo ni kioo kwa kata ya Kigonsera.
“lengo kubwa la Wakala wa Barabara za vijijini na mijini(TARURA)ni kuwawezesha wananchi wa kata ya Kigonsera na wilaya ya Mbinga kwa ujumla kupata wepesi katika shughuli zao za kila siku hasa kilimo cha mzao ya chakula na biashara”alisema.
Kwa mujibu wa Mussa, kazi zilizofanyika hadi sasa ni kujenga Barabara kwa tuta kwa kiwango cha lami ambapo mkandarasi anaendelea kujenga mitaro ya kupitisha maji eneo lote la mradi na baada ya kazi hiyo ataendelea kuweka alama za barabarani na kufunga taa.
Mkazi wa kijiji cha Kigonsera Benson Chiwinga alisema,ujio wa miradi ya Barabara unawezesha vijana wengi kupata kazi zinazowapatia kipato na kupata ujuzi ambao baada ya miradi hiyo kukamilika wanautumia kuendelea kujiajiri na kuepuka kushiriki kwenye matukio ya kiharifu.
Ameipongeza Serikali kwa kuleta miradi hiyo,lakini ameomba isichoke kuendelea kuleta miradi katika Tarafa ya Kigonsera ili wananchi waweze kunufaika kwani itawasaidia kupata ujuzi na kuboresha maisha na kukuza uchumi wao.
“Tunaipongeza sana Serikali yetu kwa hiki inachofanya kwani ni msaada mkubwa kwetu sisi Wananchi tunaoishi hasa maeneo ya vijijini,sisi tunaridhika na kufurahi kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali kupitia TARURA”alisema Chiwinga.
Haji Mbawala alisema,awali Barabara hiyo ilikuwa mbaya kutokana na kuwa a madimbwi mengi katikati ya barabara hasa wakati wa mvua hali iliyosababisha shughuli zao za kilimo na usafiri na usafirishaji kuwa ngumu.