Mkazi wa Mji wa Kitalii wa Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambaye jina lake halikufahamika mara moja akipitia na Pikipiki kwenye moja ya Barabara mpya za lami katika mji huo.
Muonekano wa baadhi ya barabara za lami katika mji wa Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma iliyojengwa na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini(TARURA)ambayo imesaidia kupendezesha mji huo na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,wakipitia kwenye moja ya Barabara za lami zilizojengwa na Serikali kupitia TARURA.
Na Mwandishi Maalum,
Nyasa
BAADHI ya wakazi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za vijijini na mijini(TARURA) kwa kuboresha miundombinu na kujenga barabara za mitaa katika mji mdogo wa Mbambabay kwa kiwango cha lami.
Wamesema,ujenzi wa Barabara hizo umesaidia kurahisisha huduma ya usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuondoa adha ya vumbi kipindi cha kiangazi na matope kila inapofika msimu wa mvua pamoja na maeneo yao kupanda thamani ikilinganishwa na siku za nyuma.
Petro Zambala mkazi wa Mbambabay alisema,uamuzi wa Serikali ya awamu ya sita kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika mji huo utaharakisha maendeleo na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya ya Nyasa.
Alisema,kabla ya barabara za lami baadhi ya huduma za kijamii zilipatikana kwa shida kwa sababu walishindwa kufika maeneo ya kutolea huduma hizo kwa wakati, jambo lililosababisha kuwa na maisha magumu.
Mkazi mwingine wa Mbambabay Nikaya Mbalale alisema,tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani kuna mabadiliko makubwa katika mji huo hasa baada ya TARURA kupatiwa fedha nyingi ambazo zimewezesha kuboresha miundombinu ya barabara zake kwa lami, tofauti na siku za nyuma ambapo barabara nyingi za mitaa zilikuwa za vumbi.
Alisema,kuimarisha na kuboreshwa kwa barabara hizo zimehamasisha na kuwavutia watu wengi kwenda kuwekeza katika Mji wa Mbambabay ambao wananchi wake wanategemea shughuli za uvuvi na kilimo ili kuendesha maisha yao.
“ni jambo la faraja kwetu sisi wananchi Serikali yetu ya awamu ya sita kutujengea barabara za lami kwenye mitaa yetu,siku za nyuma tulipata shida kubwa kupitia kwenye maeneo haya kwenda kutafuta huduma za kijamii kwenye maeneo mengine”alisema Mbalale.
Aidha Mbalale,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa mradi wa barabara ya Mbambabay- Mbinga yenye urefu wa kilometa 66 kwa kiwango cha lami.
Alisema,kukamilika kwa barabara hiyo kumesaidia kupunguza gharama za maisha na usafiri kwani hapo awali walikuwa wanalipa Sh.15,000 nauli ya kutoka Mbambabay hadi Mbinga lakini kwa sasa wanalipa Sh.9,000 hadi 10,000.
“kabla ya barabara ya lami ya Mbambabay-Mbinga,wilaya yetu ya Nyasa ilikuwa kama kisiwa kila inapofika msimu wa masika,barabara zilijifunga hivyo kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali”alisema.
Alisema,Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake imemaliza kero hiyo,sasa magari yanafika na kuondoka kwenye mji wa Mbambabay muda wowote na wananchi wanafanya shughuli zao za uzalishaji mali.
“awali kila inapofika kipindi cha masika tulikuwa kwenye mateso makubwa sana kwani barabara zote zilijifunga kutokana na ubovu wa barabara,magari pekee yaliyoweza kufika katika wilaya ya Nyasa ni LandRover tu,hali hii ilipelekea tuwe na maisha magumu sana”alisema Mbalale.
Jackob Madondola alisema,miaka ya nyuma kila inapofika msimu wa masika wananchi wa Mji wa Mbambabay walikuwa kwenye mateso makubwa kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji kutokana na kukosekana kwa mitaro ya kutiririsha maji kwenda Ziwa Nyasa.
Alisema,tangu TARURA ilipoboresha miundombinu kwa kujenga barabara za lami na mifereji ya kupitisha maji wananchi wanaishi kwa amani na wanapata muda wa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato bila hofu badala ya kubaki nyumbani pindi mvua zinaponyesha ili kuokoa mali zao zisisombwe na maji.
Alitolea mfano katika mlango wa kuingia kituo cha afya Mbambambay, kulikuwa na miundombinu mibovu ya barabara iliyokwamisha kuwahisha wagonjwa hasa akina mama wajawazito na watoto kupata huduma za haraka ili kuokoa maisha yao.
“kwa hiyo uletaji wa fedha katika wilaya yetu umesaidia sana kumaliza kero ya usafiri na usafirishaji kwa kiwango kikubwa na sasa wananchi wanaishi vizuri na kwa amani wakati wote,tunaishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kazi nzuri iliyofanya”alisema.
Kaimu meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa Derick Theonest alisema,TARURA inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kwa kujenga barabara za lami ili kuboresha mazingira na maisha ya wananchi wa mji wa utalii wa Mbambabay na wilaya ya Nyasa kwa ujumla.
Alisema,hadi sasa wamebakisha kilometa1 ili kukamilisha barabara za lami katika mji wote wa Mbambabay na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuipatia TARURA fedha kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara za lami ambazo zina mchango mkubwa katika kuchochea na kuharakisha maendeleo.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwani zinatumia fedha nyingi kuzitekeleza.