Mwenyekiti Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania Mchungaji Barnabas Ngusa akizungumzia mgogoro kati yao na Kanisa la wabaptist Tanzania uliodumu kwa miaka mitano.
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Uongozi wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania, umemwangukia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kumuomba kuingilia kati kutatua mgogoro kati yao na Kanisa la wa Baptist Tanzania uliodumu kwa muda wa miaka mitano.
Sababu ya mgogoro huo ni kubadilishwa kwa katiba na jina la dhehebu ambayo ilivuruga mwenendo na ustawi mzima wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania.
Akizungumza Leo Jumamosi Januari 18, 2025 na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania, Mchungaji Barnabas Ngusa amesema wameshindwa kupiga hatua mbalimbali ikiwemo za kimaendeleo kutokana na migogoro ambayo imeibuliwa na baadhi ya watu ambao wameanzisha Imani nyingine.
“Katiba ya 2009 ambayo tunaisimamia sisi ilikuwa inasema mali ambazo zimetafutwa na kanisa la mahali zinakuwa zinamilikiwa na kanisa la mahali hapo na jumuiya kuu inakuwa ni wasimazi wa hizo mali ili zisiweze kuporwa na watu wengine, lakini kanisa la wabaptist wao walitengeneza katiba ambayo inasema Askofu Mkuu ndio mwenye mamlaka ya kusimamia kila kitu jambo ambalo siyo sahihi”,
Amesema kwa sasa watu wanasali kwa wasiwasi kwani wanahofia kuvamiwa pindi wanapokuwa kwenye ibada.
“Hadi sasa baadhi ya makanisa yao yamefungwa na watu wanakosa pakuabudia kama ilivyokuwa kawaida yao, huku baadhi ya mali za kanisa na miradi ikichukuliwa na kubadilishwa majina na mingine kuuzwa bila ridhaa ya Jumuiya Kuu ya Baptist Tanzania ambao ndio wamiliki wa mali hizo” amesema Mchungaji Ngusa
“Kama Jumuiya tunashangaa sana watu wanapoanzisha migogoro wakati kanisa hili limekuwepo kwa muda mrefu na kunamakanisa mengi Tanzania nzima ambayo yanamiradi mingi hivyo jambo hili la migogoro limekuwa chanzo cha kuvuruga Imani yetu na kufanya miradi yetu mingi kuharibika”,
“Sisi tunachoomba walioanzisha Imani nyingine waendelee na Imani yao na sisi watuache na Imani yetu ambayo tuko nayo tangu zamani hivyo Tunamuomba Rais wetu,mama yetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atusaidie sana kumaliza mgogoro huu ambao umekuwa ukiwaathiri waumini wetu”, amesema Mchungaji Ngusa