WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 14,2025 jijini Dodoma kuelekea mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari 21 na 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Naibu Waziri Mhe.David Silinde.
WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati akizungumza kuelekea mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari 21 na 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Naibu Waziri Mhe.David Silinde.
WAZIRI wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,akizundua mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari 21 na 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Na.Alex Sonna-DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) uliopangwa kufanyika February 21 hadi 22,mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Januari 14,2025 jijini Dodoma na Waziri wa kilimo Mhe.Hussein Bashe,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo ambao umeandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO) kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.” .
Bashe amesema mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa nchi zinazolima Kahawa Barani Afrika, Mawaziri wa Kilimo, Sekta Binafsi, Viongozi wa Taasisi za Kahawa katika nchi zinazolima Kahawa, Wakulima na Wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa Kahawa.
“Mkutano huu utatoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika na Mashirika yake, Benki za Maendeleo za Afrika na taasisi nyingine za fedha ili kuunda programu zinazochochea ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Kahawa.”amesema Mhe.Bashe
Ameongeza kuwa kwa upande wa Tanzania utekelezaji huu umeanza kupitia Wizara ya Kilimo ambapo imezindua programu wa ujasiriamali kwa vijana uitwao Jenga Kesho Iliyo Bora – Build a Better Tomorrow – BBT ambapo mojawapo ya mipango inayotekelezwa ni kuanzisha “Maduka ya kahawa yanayotembea” ili kuchochea na kuongeza matumizi ya kahawa nchini,”
Hata hivyo Mhe.Bashe amesema mpango wa kuanzisha mkutano wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika ni matokeo ya azimio lililopitishwa wakati wa mkutano wa 61 wa mwaka wa IACO uliofanyika Kigali, Rwanda, Novemba 18, 2021, la kuandaa mkutano wa ngazi ya juu wa nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika ili kutathmini mapungufu na changamoto zinazosababisha kudumaa kwa wa sekta ya kahawa Barani Afrika.
“Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Mkutano wa kwanza wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika ulifanyika nchini Kenya mwezi Mei 2022, na ulipitisha “Tamko la Nairobi” (Nairobi Declaration) ambalo liliazimia kuweka mkakati wa kuingiza zao la kahawa kama bidhaa muhimu ya kimkakati katika Umoja wa Afrika (AU) sambamba na Agenda 2063 ya AU.”amesema Mhe.Bashe
Aidha amesema mkutano wa pili wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika uliofanyika Kampala, Uganda, Agosti 2023, ulipitisha Tamko la Kampala (Kampala Declaration) ambalo lilikusudia kuwaomba Wakuu wa Nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika kuunga mkono kuidhinishwa na kujumuishwa kwa zao la kahawa kama bidhaa muhimu ya mkakati katika AGENDA 2063 ya AU na kuifanya IACO kuwa shirika maalum la Umoja wa Afrika.
Katika Kikao cha 37 cha kawaida cha Baraza la kuu la umoja wa Afrika kilichofanyika Februari 2024 huko Addis Ababa, Wakuu wa Nchi na Serikali walipitisha kwa kauli moja kuingiza zao la kahawa kama bidhaa muhimu ya mkakati katika AGENDA 2063 ya AU na kuifanya IACO kuwa shirika maalum la Umoja wa Afrika.
Amesema kuwa moja ya hatua zilizochukuliwa katika kutatua changamoto za biashara ya kahawa baina ya nchi za Afrika ni kuanzishwa kwa Mkataba wa Biashara Huria Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA) wa 2018 kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara katika ya nchi za Africa na hivyo utekelezaji kamili wa mkataba huo utaimarisha biashara ya kahawa bila vizuizi baina ya nchi za Africa.
Hivyo, Mkutano huu wa Tatu utajadili maeneo muhimu katika mnyororo wa thamani wa kahawa kwa ajili ya kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana.