Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile kushoto,akikabidhi misaada mbalimbali kwa Diwani wa kata ya Seedfarm Manispaa ya Songea Festo Mlelwa kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo waliotahirika na maafa ya mvua iliyoambatana na upepo mkali tarehe 28 Desemba 2024 na tarehe 2 Januari mwaka huu,kushoto Katibu wa CCM Songea mjini James Mgego.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kuchile kata ya Seedfarm Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Ali Kuchile kulia,akipokea baadhi ya vitu kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile kushoto, kwa niaba ya wananchi wa mtaa huo walioathirika na maafa ya upepo yaliyotokea tarehe 28 Desemba mwaka jana na tarehe 2 Januari mwaka huu.
Na Mwandishi Maalum,Songea
WAATHIRIKA wa maafa yaliyotokana na mvua pamoja na upepo mkali tarehe 28 Desemba 2024 na Tarehe 2 Januari mwaka huu wilayani Songea mkoa wa Ruvuma,wameanza kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa Serikali ya wilaya ya Songea na na wadau mbalimbali.
Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile alisema,maafa hayo yamebomoa nyumba zaidi ya 155 ambapo katika Halmashauri ya Madaba nyumba 15 zimebomoka,Songea vijijini nyumba 7 na katika Manispaa Songea nyumba zilizobomoka ni 133.
“hizi nyumba zimebomoka kwa maana ya paa zake kuezuliwa na nyingine kuanguka kabisa,pia kuna shule zetu mbili ambazo ni shule ya Sekondari ya wavulana(Songea Boys) na shule ya Sekondari Chandarua”alisema Dc Ndile
Alisema,baada ya tukio kamati ya maafa ya wilaya ya Songea ilikutana na kufanya tathimini ya kujua ukubwa wa tatizo na katika hatua ya kwanza walibaini hasara iliyotokea ni kubwa japo hakuna mwananchi aliyepoteza maisha.
Ndile alisema,wamepokea fedha taslimu zaidi ya Sh.milioni 4,unga wa mahindi kilo 2120,sukari kilo 40,mchele kilo 380,maharage zaidi ya kilo 200,mafuta ya kula,maturubai 200,chumvi kilo 200 na sabauni yaliyotolewa na wadau mbalimbali.
Amewashukuru wadau kwa kusaidia waaathirika ikiwemo kampuni ya Aviv Ltd iliyotoa mchele zaidi ya 2,000,maharage na maturubai ambayo yatawasaidia waathiri kujihifadhi wakati huu ambao utaratibu mwingine unaendelea kufanyika kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika.
DC NdileaAmewaagiza wenyeviti wa mitaa na vijiji waliopokea msaada huo kwa niaba ya waathirika,kuhakikisha misaada hiyo inawafikia walengwa bila kupotea na Serikali itawachukulia hatua kali kiongozi atakayeshindwa kufikisha misaada hiyo kwa walengwa.
Alisema,Serikali imejaribu kufanya kila inaloweza kwa ajili ya kupata misaada hiyo ili kuwasaidia binadamu wenzetu waliopatwa na janga hilo ambalo limewarudisha nyuma kimaisha.
Katibu wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Kelvin Challe,amewaomba wadau wengine walioguswa na tatizo hilo kujitokeza kuwasaidia wananchi wenzao katika kipindi hiki kigumu ambacho bado wanahitaji msaada wa hali na mali.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Songea mjini James Mgego,amewataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Diwani wa kata ya Seedfarm Festo Mlelwa,amempongeza Mkuu wa wilaya kwa kukusanya misaada hiyo na kuwashukuru wadau wote waliochanga pamoja na Serikali kwa kuratibu na kusimamia zoezi zima la ukusanyaji na ugawaji wa misaada.
“naipongeza serikali ya wilaya ya Songea na wadau wote kwa kuwashika mkono wananchi wa kata yangu na kata nyingine walioathirika na mvua pamoja na upepo mkali uliopelekeaa baadhi ya mali ikiwemo nyumba kuharibika”alisema.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kuchile kata ya Seedfarm Manispaa ya Songea Ali Shafii Kuchile,amehaidi misaada yote itafika kwa walengwa na kusimamia vizuri ugawaji wa vifaa hivyo kwa waathirika.