Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas kushoto,akipanda mti wa mbao kwenye viwanja vya Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma wakati wa uzinduzi wa upandaji miti ambapo mkoa huo unatarajia kupanda miti milioni 6.9 kwa mwaka 2025,kulia ni Mhifadhi wa misitu kutoka wakala wa huduma za misitu(TFS)wilaya ya Songea Issa Mlela.
Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)kanda ya kusini Manyise Mpokigwe kushoto,akiwaongoza wahifadhi wa misitu kutoka wilaya mbalimbali za kanda ya kusini kukagua bustani ya miti iliyopo katika eneo la milima ya Matogoro Manispaa ya Songea.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,kulia akipanda mti wa matunda kwenye safu za milima ya matogoro katika manispaa ya Songea baada ya kuzindua rami zoezi la upandaji miti kimkoa ambapo jumla ya miti 6.9 inatarajia kupandwa katika mkoa huo,kushoto Mhifadhi wa misitu wa TFS Wilaya ya Songea Issa Mlela.(Picha na Muhidin Amri).
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akimwagilia mti maji baada ya kupanda kwenye safu za milima maarufu ya Matogoro katika Manispaa ya Songea,anayeshuhudia katikati Katibu Tawala wa mkoa huo Mary Makondo na kushoto Mhifadhi misitu wa TFS wilaya ya Songea Issa Malela(Picha na Muhidin Amri)
Na Mwandishi wetu,Ruvuma
MKOA wa Ruvuma,umezindua zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma(Homso) iliyopo eneo la Mwengemshindo Manispaa ya Songea ambapo miti zaidi ya 30,000 imepandwa kuzunguka Hospitali hiyo.
Kwa mwaka 2025,mkoa wa Ruvuma umepanga kupanda miti milioni 6,985,574 aina mbalimbali katika wilaya zake zote tano kama mkakati wa kukabiliana na uharibu wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi,kupendezesha manzari ya mkoa huo kupitia Halmashauri zake na kuufanya kuwa wakuvutia.
Mkuu wa mkoa huo Kanali Ahmed Abbas, ameipongeza wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) kanda ya Kusini kutokana na jitihada zake za kupanda miti na utunzaji mazingira katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Hata hivyo,ameitaka TFS kuhakikisha zoezi la upandaji miti linakuwa endelevu kutokana na umuhimu wake na miti inayopandwa inalindwa na wananchi kujenga tabia ya kupanda miti na kutunza mazingira katika maeneo yao.
Katibu Tawala wa mkoa huo Mary Makondo alisema,kama mkoa unaandaa andiko ambalo litafanya suala la upandaji miti kuwa sehemu ya mpango mahususi ili mkoa huo uwe wa kijani wakati wote badala ya kusubiri hadi siku maalum ya upandaji miti.
Kwa upande wake Kamanda wa wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwe alisema,mwaka huu wamepanga kupanda miti 2,760,000 katika mikoa mitatu ya kusini yaani Lindi Mtwara na Ruvuma na miti itakayopandwa imeoteshwa kwenye vitalu vyake.
Alisema,watahakikisha katika msimu huu wa mvua miti iliyooteshwa kwenye vitalu vya TFS itapandwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye taasisi za Serikali na mingine itatolewa bure kwa watu binafsi ili waanze kupanda miti kibiashara kwa kuwa miti ni uchumi mkubwa kuanzia ngazi ya familia,wilaya,mkoa na Taifa.
Kamanda Mpokigwe,amewahimiza wananchi wa mikoa ya kusini,kwenda ofisi za TFS ngazi ya wilaya kuchukua miche kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao ili kujiongezea kipato ili kuondokana na umaskini.
Mhifadhi misitu(TFS) wa wilaya ya Songea Issa Mlele alisema,kwa mwezi Januari pekee miti zaidi ya 1,290,000 itapandwa kwenye vyanzo vya maji,taasisi za Serikali ikiwemo shule za msingi na sekondari,zahanati,vituo vya afya,Hospitali na maeneo ya umma.
Alisema,wilaya ya Tunduru itapandwa miti 1,100,000 kati ya hiyo miti ya mbao 600,000,miti 200,000 itapandwa kwenye vyanzo vya maji na miti ya matunda ni 500,000 na wilaya ya Namtumbo miti 539,000 ni ya mbao,miti 50,000 itapandwa kwenye vyanzo vya maji na miti 17,000 ya matunda.
Aidha Mlela,alitaja maeneo mengine yatakayonufaika na mpango huo ni pamoja Halmashauri ya wilaya Mbinga ambapo miti ya mbao itakayopandwa ni 350,000 miti 150,000 itapandwa kwenye vyanzo vya maji na miti 250,000 ya matunda na kuwa na jumla ya miti 750,000.
“katika Halmashauri ya mji Mbinga tunatarajia kupanda miti ya mbao 1,200,000,miti ya vyanzo vya maji 250,000 na miti ya matunda 59,000 hivyo kufanya miti yote tutakayopanda kwa Halmashauri ya Mji Mbinga ni 1,509,000”alisema Mlela.
Kwa upande wa Halmashauri ya Madaba Mlela alisema,watapanda jumla ya miti 535,000 kati ya hiyo miti ya mbao ni 500,000,miti ya vyanzo vya maji 23,000 na miti ya matunda 12,000 na kwa upande wa Manispaa ya Songea watapanda miti 363,700 ambapo miti ya mbao ni 320,000 miti 27,000 ya vyanzo vya maji na miti 16,700 miti ya matunda.
Mlela alieleza kuwa,kwa Halmashauri ya wilaya Songea wanatapanda miti ya mbao 484,701 miti 127,652 ya vyanzo vya maji,miti ya matunda 389,251 na katika Halmashauri ya Nyasa watapatanda miti 1,320,000 ambapo miti 1,300,000 ya mbao,miti 400,000 ya vyanzo vya maji na miti ya matunda 16,000.