Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENYEKITI mpya wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Hans Nkya amewataka wajumbe wa mamlaka hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha ili waweze kuyapatia majawabu matatizo ya jamii inayowazunguka.
Nkya ameyasema hayo wakati akitoa hotuba yake ya mwanzo ya shukurani mara baada ya wajumbe wote 35 wa mamlaka hiyo kupitia CCM kumpitisha kwa kura zote 35 za ndiyo.
Amesema jamii ya Mirerani ina changamoto mbalimbali kwenye sekta ya elimu, afya na huduma nyingine hivyo wanapaswa kuzipambania ili majawabu ya jamii yapatikane.
Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano wa wajumbe wote wa mamlaka hiyo wataweza kupambana na kutatua matatizo tofauti ya watu wa eneo hilo hivyo wanapaswa kuwa kitu kimoja.
“Sitakuwa na mtoto wa mgongoni wala wa mabegani wote mna haki sawa kwangu, hii nafasi nimepewa kama koti tuu nikihisi joto nalitoa na kukaa pembeni hivyo tushirikiane kuijenga Mirerani,” amesema.
Amesema wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wamemuamini na kupenda awaongoze awe mbele yao na siyo kwamba yeye ana akili nyingi au uwezo mkubwa kuliko wote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa mamlaka ya mji huo, Adam Kobelo amesema uchaguzi umepita hivyo wajumbe wagange yajayo kwa mustakabali wa Mirerani.
“Nipende kumpongeza Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer kwa kutumia maneno ya busara katika mchakato wa uchaguzi,” amesema Kobelo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota, amesema ameusimamia uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu wake na umefanyika vyema.
Amesema uchaguzi umekuwa rahisi kwani Mwenyekiti na Makamu wake wote ni wa chama kimoja hivyo umefanyika kwa muda mfupi na salama, kinachofuata viongozi wakafanye kazi.
”Changamoto zilizoongelewa hapa tutazichukua na zile ambazo tutaweza kuzitekeleza zitafanyiwa kazi kwa lengo la kuhakikisha maendeleo yanapatikana,” amesema Makota.
Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia amesema wajumbe hao wana kazi kubwa ya kuhakikisha sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu inaboreshwa.
Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi amesema hivi sasa uchaguzi wa mamlaka hiyo umeshafanyika hivyo ni matarajio yake kuhakikisha wajumbe wanapanga maendeleo.
Diwani wa Kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amesema wajumbe hao wanapaswa kutanguliza mbele maslahi ya jamii inayowazunguka ili waweze kupiga hatua ya maendeleo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Amos Shimba amewaasa wajumbe hao kuhakikisha maridhiano na maendeleo kupitia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan yanapatikana kwa jamii.