Timu ya waendesha pikipiki zenye miguu mitatu maarufu Bajaji imeibuka mshindi wa mashindano ya Ilemela Christmas Bonanza kwa mwaka 2024 baada ya kuifunga timu ya wasanii magoli mawili kwa moja mchezo uliochezwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
Akizungumza mara baada ya kuisha kwa mchezo huo, Mratibu wa Ilemela Christmas Bonanza Ndugu Fidelis Irengo amesema kuwa mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amekuwa na utaratibu wa kuandaa bonanza la kila mwaka kinapofika kipindi cha sikukuu ya Christmas na mwaka mpya ili kuwakutanisha wananchi wa Jimbo hilo pamoja na kusheherekea sikukuu huku watoto wanaosoma shule za msingi na sekondari wakipatiwa zawadi mbalimbali ikiwemo madaftari, kalamu, na vifaa vyengine vya shule
‘.. Mhe Dkt Angeline Mabula ameweka utaratibu wa kushiriki pamoja sikukuu za mwisho wa mwaka ambao tunakuwa na bonanza la michezo mbalimbali kwa watoto na wakubwa ili kutoa fursa ya watu kukaa pamoja na kushirikiana katika kuzijadili, kutatua kero na changamoto zinazotukabili kwa pamoja ..’ Alisema
Aidha Ndugu Fidelis ameitaka jamii kuendelea kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zao, kujipatia ajira na burudani
Nae nahodha wa timu ya Bajaji Bwana Ecko Charles amefafanua kuwa timu yake imeweza kufanya vizuri katika bonanza hilo ni kwasababu imekuwa na mazoezi ya kutosha kwa muda mrefu huku akimpongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kushirikisha timu yao katika mashindano ya Jimbo Cup pamoja na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo
Kisendi Alfred ni nahodha wa timu ya wasanii ambapo amesema kuwa pamoja na timu yake kushindwa kufanya vizuri katika mchezo huo lakini wamepata manufaa makubwa ikiwemo kujuana na kubadilishana zoefu mbalimbali zitakazosaidia kujikwamua kiuchumi
Ilemela Christmas Bonanza 2024 lilifikia kilele chake kwa kugawa zawadi za sikukuu ya Christmas kwa watoto na burudani kabambe ya muziki katika viwanja vya Furahisha