Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi Abdi Makange akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana kwenye Mahafali ya 14 Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi.
Wahitimu wakiwa ukumbini
Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi Abdi Makange akitoka cheti kwa mhitimu katika Mahafali ya 14 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi Jijini Mwanza.
Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi Abdi Makange (katikati) akitoa cheti kwa mhitimu kwenye Mahali ya 14 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi Jijini Mwanza.
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi, Dongo Nzori akitoa taarifa ya Chuo hicho kwenye Mahafali ya 14
Na Hellen Mtereko
Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi Jijini Mwanza ( MISUNGWI CDTTI) wamesisitizwa kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwaujumla.
Msisitizo huo ulitolewa Jana Ijumaa Disemba 20, 2024 na Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Abdi Makange kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana kwenye mahafali ya 14 ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano chuoni hapo.
Pamoja na msisitizo huo pia aliwaasa wahitimu kufanya kazi kwa weredi,uadilifu,uaminifu na umakini hatua itakayo saidia kulinda hadhi ya Chuo chao na Wizara.
“Nawaasa popote mtakapobahatika kupata fursa ya kufanya kazi za kuajiriwa na kujiajiri fanyeni kazi kwa uaminifu mkubwa na kwakujituma ili muweze kuitumikia nchi yenu kwa heshima, tambueni kuwa rushwa ni adui wa haki hivyo mkiiendekeza mtajenga miundombinu iliyo chini ya viwango ambayo inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii”, Alisema Makange
Kwaupande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Mh. Alexander Mnyeti aliwaomba wahitimu kuachana na dhana ya kusubili ajira badala yake wachangamkie fursa ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
“Kwa sasa ziwa letu halina samaki wa kutosha hivyo mnapaswa kujiunga kwenye vikundi vya ujasiliamali ili muweze kupata mikopo inayotolewa na Serikali ambayo itawawezesha kutengeneza vizimba vya kufugia samaki ambapo baada ya miezi minane mnaanza kunufaika”, Alisema Mnyeti
Awali akisoma taarifa ya Chuo hicho Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Bw. Dongo Nzori alisema kwa mwaka wa masomo 2023/2024 chuo kilikuwa na wanafunzi 602 kati yao wanaume367,wanawake 235 na watumishi 16.
Alisema ongezeko hilo linatokana na uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya Chuo,kupangiwa wanafunzi wa moja kwa moja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) pamoja na uendelezaji wa program tatu za uanagenzi,ushirikishaji jamii na kituo cha ubunifu na maarifa ambazo zimekuwa na mwitikio chanya katika kukitambulisha chuo.
Nzori alieleza kuwa kumekuwa na ongezeko la wahitimu wanawake tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 1984 ambapo wahitimu wa kike walikuwa sita sawa na asilimia 0.12 ya wahitimu wote.
“Katika mahafali haya kuna wahitimu wanawake 221 sawa na asilimia 39 chuo kinajivunia kuwa sehemu ya mchango wa kuwainua wanawake katika elimu,ujuzi na kusaidia taifa kuleta mchango chanya katika maendeleo ya ujenzi na kada ya uhandisi ujenzi kwa ujumla”, alisema Nzori
Aidha, alieleza kuwa mwaka wa masomo 2024/2025 chuo kipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha program nyingine ya Uhandisi Maji na Maendeleo ya Jamii ambayo imeandaliwa kwa kufuata taratibu na Sheria za NACTVET.
“Program hii itaiwezesha chuo kujipanua zaidi na kusaidia taifa kuongeza wataalamu katika fani mbalinbali za ujuzi na teknolojia na hii itaongeza udahili zaidi”,Alifafanua Nzori