Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini Mheshimiwa Emanuel Mwakasaka ( wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye maandamano ya Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora hivi karibuni.
Wakazi wa Jimbo la Tabora Mjini wakimsikiliza Mbunge wao Emanuel Mwakasaka na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika Kata ya Cheyo Mjini Tabora.
Na Lucas Raphael,Tabora
MBUNGE wa Jimbo la Tabora Mjini Emanuel Mwakasaka amemwomba Waziri wa Afya Jenista Mhagama kutekeleza ahadi ya serikali ya kukipatia Kituo cha Afya Town Kliniki kiasi cha shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto.
Alitoa kauli hiyo jana ya ombi la hilo alipokuwa akiongea na mamia ya wakazi wa Kata ya Chemchem na Kata jirani zilizopo katika manispaa hiyo wakiwemo wanaCCM katika mkutano wa hadhara .
Mwakasaka alisema kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa ya kuboresha huduma za kijamii katika Jimbo hilo na maeneo mengine hali ambayo imesaidia kupunguza kero za wananchi.
Aliongeza kuwa ni dhamira ya serikali ya awamu ya 6 kuona vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinakuwa na miundombinu inayotakiwa, ndiyo maana serikali ikaahidi kuleta kiasi hicho cha fedha ili kujengwa jengo hilo.
‘Ahadi hiyo bado ipo hadi sasa ila haijatekelezwa, na ahadi ni deni, ninawaahidi kuwa nitalifikisha kwa Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, huyu ni jembe la kazi, naamini atatuletea kiasi hicho na Jengo hilo la kisasa litajengwa’, alisema Mwakasaka.
Mwakasaka alimpongeza Rais Samia kwa kuwaletea magari 2 mapya ya kuhudumia wagonjwa (ambulance) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Kitete na zaidi ya sh bil 2 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo.
Aidha alieleza kufurahishwa na uamuzi wa serikali wa kuleta kiasi cha sh bil 19 kwa ajili ya ujenzi wa Tawi la Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika Jimbo hilo, mkataba wa ujenzi tayari umesainiwa ili kuanza kazi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Elisha Nkambaku aliwapongeza wanaCCM na wananchi wote kwa kuendelea kukiamini chama hicho na serikali yake na kuwapigia kura za kushindo wagombea wa CCM.
Alibainisha kuwa katika uchaguzi huo CCM ilipata ushindi wa asilimia 95 kwenye Serikali za Mitaa, asilimia 98 Serikali za Vijiji na asilimia 98 nafasi za Vitongoji, na kubainisha kuwa matokeo hayo ni ishara ya kukubalika zaidi kwa chama hicho.
Nkambaku alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuwa karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia katika maeneo yao ikiwemo kutatuliwa kero zinazowakabili.