Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew,akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji linalojengwa katika eneo la Chandamali katika Manispaa ya Songea.
Na Mwandishi Wetu,Songea
ZAIDI ya vijiji 10,000 sawa na asilimia 79.8 kati ya vijiji 12,333 vimepata maji safi na salama huku huduma ya maji ikiongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 79.9 mwaka 2024 tangu Serikali ilipoanzisha wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mwaka 2019.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa maji Mhandisi Kundo Mathew,wakati akizungumza na viongozi wa Serikali ya mkoa wa Ruvuma akiwa kwenye siku ya kwanza ya ziara ya siku mbili mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kundo ni kwamba,katika kipindi hicho wizara ya maji imetekeleza na kukamilisha jumla ya miradi 164 kati ya 177 ambayo haikukamilika katika awamu zilizopita licha ya Serikali kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.
Amewahakikishia wananchi kuwa,wizara ya maji imejipanga kufikisha huduma ya maji safi na salama kwenye vijiji vyote hapa nchini na hakuna Mwananchi atakayekosa huduma ya maji kwenye makazi yake.
“Wizara yetu ikiongozwa na Waziri Jumaa Aweso tumejipanga kwa kuendelea kufanya uchambuzi na kutambua miradi gani itakayotoa majibu ya kero ya maji kwa wananchi kupitia miradi ya kawaida,miradi ya miji 28 na miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini,nawatoa wasiwasi na kuwahakikishia kwamba hakuna mradi wa maji utakaosimama”alisema Naibu Waziri Kundo.
Alisema katika kufanikisha mpango huo,watatumia vyanzo vilivyopo ikiwemo mto Ruvuma,ziwa Tanganyika na ziwa Nyasa kuiunganisha Tanzania katika mfumo mzima wa maji ili maji yatakayozalishwa yatumike kuharakisha kukua kwa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha alieleza,wizara ya maji inakusudia kutengeneza gridi ya Taifa ya Maji ambayo chanzo chaka ni Ziwa Victoria na gridi hiyo itakapokamilika wataanza kuzalisha maji taka kwani kwa kawaida yanapozalishwa maji safi,asilimia 80 yanabadilika kuwa maji taka.
Akizungumzia mradi wa uchimbaji visima 900/5 kwa kila jimbo Kundo alisema,tayari wameanza utekelezaji wake ambapo mkoa wa Ruvuma umepata visima 40 ambavyo vitakapokamilika vitapunguza kero ya huduma ya maji na wananchi watapata muda mwingi kwenda kufanya kazi za kujiletea maendeleo badala ya kutafuta maji.
Alisema,visima vitakavyokuwa na maji mengi Wizara itajenga miundombinu ili maji hayo yapelekwe kwenye vijiji vya jirani ili Watanzania wote waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali yao kwenye sekta ya maji.
Naibu Waziri Kundo alisema,wizara hiyo imeanza kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufunga mita za maji za lipa kabla ya matumizi(Pre paid) kwenye taasisi mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
Alisema,hatua hiyo itamaliza malalamiko ya wananchi kuhusu kubambikiwa ankara za maji na kuhakikisha taasisi hizo zikiwemo za majeshi zinalipia gharama ya maji kulingana na matumizi yake.
Kaimu meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Ruvuma Batholomeo Matwiga alisema,upatikanaji wa huduma ya maji vijijini ni asilimia 70.9 ambapo watu 997,685 wanapata huduma ya maji safi na salama wakati malengo ni kufikisha asilimia 85 kwa wakazi waishio vijijini na asilimia 95 waishio mjini ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa, mahitaji ya maji katika mkoa huo ni mita za ujazo 44,119.14 kwa siku kwa wastani wa lita 25 kwa mtu mmoja wakati uzalishaji wa maji ni lita 31,994 ambazo zinahudumia watu 973,833 waishio vijijini.
Alisema,mwaka wa fedha 2023/2024 walitengewa Sh.bilioni 22.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, lakini hadi kufikia tarehe 30 Juni 2024 walipokea Sh.bilioni 14. 6 na mwaka 2024/2025 wametengewa Sh.bilioni 18.9 ambapo hadi tarehe 10 Disemba 2024 wamepokea Sh.bilioni 3.1 sawa na asilimia 10.7.
Katika hatua nyingine Matwiga alisema,hadi kufikia Mwezi Disemba 2024 miradi 23 yenye thamani ya Sh.bilioni 25.9 imekamilika kwa asilimia 99 na wananchi zaidi ya elfu sitini na nane wanapata huduma ya maji safi na salama kwenye vijiji 36.
Pia alisema,kulikuwa na miradi 30 inayoendelea kutekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 58.5 lakini hadi kufikia mwezi Disemba 2024 ni Sh.bilioni 19.6 zimepokelewa kati ya Sh.bilioni 58.5 kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na itakapokamilika itahudumia wananchi 268,742 kwenye vijiji 78 na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 70.9 ya sasa hadi kufikia asilimi 87 mwaka 2025.
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Joel Mbewa,ameipongeza wizara ya maji kwa kwa jitihada inazofanya kumaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama katika vijiji mbalimbali mkoani Ruvuma.