Na Silivia Amandius,
Kagera.
Wakazi wa Mkoa wa Kagera na wale wanaoishi nje ya mipaka ya Tanzania wanatarajiwa kushiriki tamasha kubwa la Ijuka Omuka, linalolenga kujadili na kuhamasisha fursa za uwekezaji katika mkoa huo. Tamasha hili litafanyika kuanzia Desemba 18 hadi 26 na litajumuisha maonesho ya kibiashara, burudani, pamoja na utambulisho wa utamaduni wa wakazi wa Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amesema kwamba tamasha hilo linalenga kukuza uchumi wa mkoa kwa kuwaleta pamoja wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuchangia mawazo juu ya maendeleo ya sekta muhimu kama viwanda na utalii.
“Tamasha la mwaka jana lilikuwa na mafanikio ya awali, lakini mwaka huu tunalenga kufanikisha maonyesho makubwa zaidi na kuhusisha wadau wengi zaidi ili kuangalia namna ya kuimarisha uchumi wa mkoa,” alisema Mwassa.
Ufunguzi rasmi wa tamasha utafanyika Desemba 19 ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, atakuwa mgeni rasmi. Tamasha hilo pia litatangazwa kwa burudani za wasanii mbalimbali, vyakula vya asili vya Kagera, na vionjo vya kiutamaduni ambavyo vinaendelea kudhihirisha urithi wa mkoa huo.
Hii ni fursa muhimu kwa wawekezaji na wadau kushirikiana kwa nia ya kuinua uchumi wa Kagera, sambamba na kudumisha utamaduni wa watu wake.