Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa amewasisitiza watumishi wa wizara hiyo kuendelea kutekeleza miradi iliyopangwa ambayo ni miongoni mwa miradi inayokuza ajira na uchumi wa nchi.
Katibu Mkuu Msigwa amesisitiza hayo, Desemba 13, 2024 Mtumba jijini Dodoma katika kikao chake na watumishi hao, ambapo amesisitiza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Hii ni wizara yenye dhamana ya kutoa habari kwa umma, kuhakikisha Watanzania wanaburudika na kupata kipato kupitia sanaa na utamaduni, na kwa sasa tunaiita ni wizara ya AFCON, hivyo kwa pamoja tunatakiwa kuhakikisha hilo linafanyika kwa maslahi ya nchi.” Amesema Ndg. Msigwa.
Amewataka watumishi kila mmoja kuhakikisha anakuwa sehemu ya utekekezaji wa majukumu ya wizara hiyo katika sekta zake zote nne.
Kwa upande wa watumishi waliopata nafasi ya kutoa maoni na kuuliza maswali, walimpongeza Katibu Mkuu huyo kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo pamoja na kuongezewa majukumu ya kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, wakiahidi ushirikiano zaidi.