Na Paul Mabeja, DODOMA
BAADA ya serikali kuzindua mpango kazi wa kitaifa wa haki na ustawi kwa watu wenye ualbino wadau wamejitokeza kupongeza hatua hiyo huku wakidai kuwa kama utasimamiwa vizuri utakwenda kukomesha mauaji ya watu wenye ualbino nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojihusisha na kusaidia watu wenye ulemavu mkoani hapa ya FDH, Maiko Salali, alisema hayo juzi wakati akitoa tamko la kuipongeza serikali kufanikisha mpango huo.
“Ni imani yetu kuwa mara baada ya kuzinduliwa kwa mpango huu, tutakwenda kutatua changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili watu wenye ualbino nchini na kulifanya kundi hili kulifurahia taifa lao sawa na watu wengine walioko katika taifa hili”alisema Salali
Aidha, alisema watu wenye Ualbino nchini kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mitazamo hasi kwa jamii.
Alisema mitazamo hiyo potofu inasababisha watu wenye ualbino kupata madhira mbalimbali ikiwemo mauwaji, kukatwa viungo na aina nyingine nyingi za ukatitili.
“Hivyo ni matarajio yetu watu wenye ualbino nchini kuwa kama mpango kazi huu wa kitaifa wa haki na ustawi kwa watu wenye ualbino nchini utasimamiwa vizuri na serikali kwa kushirikiana na wadau wegine tutafanikisha kukomesha mauaji ya kundi hilo.
“Na kupunguza matukio mengine ya kikatili ikiwemo wenye ualibino kukatwa viongo vyao kama ambavyo imekuwa ikilipotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana tuu imani potofu za kishirikina”alisema Salali
Kadhalika, alipongeza serikali kwa kufanikisha mpango huo muhimu kwa ustawi wa watu wenye ualbino na taifa kwa ujumla.
“Napenda kutumia fursa hii kwa mara nyingine, kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kupitia ofisi yake ambayo imeratibu na kufanikisha mpango kazi huu.
Aidha tunampongeza sana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete kwa kuongoza vema mchakato wote wa kufanikisha mpango huu kupitia kitengo cha watu wenye ulemavu kilichopo chini ya ofisi yake”alisema
Vile vile, alisema FDH inawashukuru wadau wote wakiwemo Chama cha watu wenye ualbino Tanzania(TAS), Standing Voice, Shirika la Umoja wa mataifa la mazingira (UNEP) na wengine wote walijitolea kuweka nguvu, rasilimali fedha na mchango wao wa kimawazo ambao umefanikisha mpango kazi huo.
Mpango kazi wa kitaifa wa haki na ustawi kwa watu wenye ualbino ulizinduliwa Disemba 3, 2024 Dar es Saalam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa bungeni baada ya maauji ya mtoto wenye ualbino katika kijiji cha Bulamula wilayani Muleba mkoani Kagera Asimwe Novath (2).