Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkoa wa Pwani umeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 413 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Akitoa taarifa ya bajeti na utekelezaji wake katika kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC), kwa niaba ya Ofisa Mipango wa Mkoa wa Pwani, Grace Tete alibainisha kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 230.5 zitatumika kwa ajili ya mishahara, shilingi bilioni 89.9 kwa maendeleo, na shilingi bilioni 68.7 ni mapato ya ndani ya halmashauri.
“Kwa matumizi ya kawaida, tumepokea shilingi bilioni 93.08. Hadi kufikia Oktoba 2024, shilingi bilioni 9.5 zimetumika kutekeleza shughuli za maendeleo, ambayo ni sawa na asilimia 105.8 ya shilingi bilioni 8.9 zilizopangwa kutolewa kulingana na makusanyo,” alisema Grace.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Grace alieleza kuwa halmashauri zimechangia shilingi bilioni 2.09, na jumla ya vikundi 138 vimesajiliwa hadi Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, alitaja changamoto zinazoukabili mkoa kuwa ni uchache na uchakavu wa magari, upungufu wa miundombinu, vifaa vya kazi, na uhaba wa watumishi hasa katika sekta za afya, kilimo, na maofisa ugani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, aliishukuru Serikali kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa maendeleo na utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani humo.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kukabiliana na changamoto za usafiri kwa watendaji wa Serikali.
Alieleza kuwa mkoa huo umepokea magari manne kwa ajili ya wakuu wa wilaya, na kuwakabidhi hivyo kuwa na magari ya wakuu wa wilaya sita ambao wamekabidhiwa magari hayo hadi sasa.
“Tuna uhaba wa vitendea kazi, lakini hali si mbaya sana. Tunapokea vifaa mara kwa mara, ikiwemo magari na pikipiki, na hii inatufanya tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi,” alisema Kunenge.